Thursday, 21 July 2011

UTAMADUNI WA KUTOWAJIBIKA, KULEANA, KUOGOPANA NA KUONEANA HAYA

Waafrika tuna tamaduni nyingi ambazo japo hatupendi watu watuambie ama watukumbushie kuwa tunazo zimesababisha udumavu wa maendeleo katika taswira nzima ya maisha jamii yetu. Utamaduni wa kutowajibika katika majukumu tunayojipa sisi wenyewe ama tunayopewa na watu wengine. Hatuna uchangamfu katika kazi yeyote ile tunaona kufanya kazi ni kupoteza muda ambao tungeutumia vizuri kupumzika huku tukinywa vinywaji tunavyopenda na tukiwa katika mazingira ya starehe.

Kuanzia muuza chipsi na mtengeneza kandambili uswahilini mpaka mawaziri katika mawizara hali ndio hiyo hata kama mtabisha maana hili la ubishi sisi ni nambari moja. Tutabisha hata kama jambo liko wazi kama jua la mchana wa saa sita. Tunafanya kazi bila ya umakinifu yakinifu bila ya shauku ya kuboresha tulilofanya jana tutalirejea leo kama ilivyokuwa jana. Tunafanya kazi kama mashine (robot) hatutumii fikra zetu kuboresha huduma ila tuna ubunifu mkuu wa kupindisha miongozo ili tupate njia ya kutoza rushwa kwa huduma tunazotoa.

Uswahilini mpaka maofisini na viwandani na hasa serikalini tuna utamaduni wa kuleana na kuogopana. Wengi wenu mnaona makosa yanayofanyika katika sehemu zenu za kazi lakini ulezi umewazidi na mnaona kwamba mkisema juu ya kosa hilo basi mtakosana na mkosaji na kwasababu hakuna mazingira ya kuadabishwa basi bora tu mgawane makosa. Hii huzaa woga kwamba wewe una siri ya Yule na Yule ana siri yako kwa hiyo wote mnakaa kimya na kulindana kwasababu ya woga wa kuvuja kwa siri mlizowekeana.

Hii huleta kushuka kwa ufanisi kazini na pia uvunjaji mkubwa wa sheria za kazi na watu kujifanya miungu watu. Unakwenda kupata huduma ambayo unalipia lakini unajikuta kama vile ile huduma umepewa bure kutokana na dharau na usumbufu utakaopata. Ukienda mahospitalini makarani hujifanya ndio madokta kwa maana bila ya kuwapa kitu kidogo huwezi kumuona dokta. Mara utaambiwa faili lako limepotea wakati ulilifungua dakika kumi zilizopita. Una ugonjwa wa kufa utaambiwa daktari hayupo lakini ukitoa kidogo kama miujiza daktari anatokea.

Hata ukienda madukani kununua bidhaa wauzaji wanakupa dharau kama vile hizo bidhaa unanunua kwa bei ya bure na wao wanakufanyia hisani kukuuzia.
Ukienda wizara ya mambo ya ndani huko ndio usitoe pua kabisa kuomba passport imekuwa ni mradi unaojenga mahekalu mbezi na kwengineko. Utaambiwa wewe si mtanzania hapo ndipo utakapo koma, unaweza kuhisi wewe ni mkimbizi kwenye nchi yako wakati wachina wanakupita na mikoba ya baba Kambarage.
Alama za vidole huchukuliwa wahalifu ili wapate kutambulika kirahisi wanaporudia makosa.Kuomba pasi ya kusafiria imekuwa kosa ama wewe ni mhalifu mtarajiwa na utajiuliza sasa haya madole mnayochukua ni ya faida gani wakati mijambazi kibao na mijizi iliyojaa mtaani hamujawahi kuikamata kwa kutumia alama za midole hii wajameni...hii ni kutokana na utamaduni wetu wa kuogopana tunaogopa kuwaambia wamarekani na ndugu zake kuwa hatuwezi kuuza alama za wananchi wetu kwa bei ya dola moja.

Tunaoneana haya kiasi watu wamekuwa wakitovuka adabu kupita mifano kwasababu wanajua na wewe unajua kuwa huwezi kumfanya kitu.hii ni kama maigizo ya Simba kumuogopa Swala..ni hivi hivi nchi inazama tunaoneana haya kuambizana kwamba ili mashua yetu iende mbele inabidi tupige makasia. Wakubwa wanakula marushwa halafu wanawekeana viporo mara kimya kama ubaridi wa asubuhi unapopiga usoni na ukaendelea kuvuta shuka.

Kwa utamaduni huu maendeleo hayaji n’go kama mvua jangwa la sahara tutaendelea kuungua na jua mpaka dunia ibadili egemeo. Yangu ni macho ila utamaduni huu utatupeleka pabaya maana wanaofaidi ni wachache na wengi tunaumia. Wengi tunaingia makanisani na misikitini ili tuonekane tuna dini lakini ukweli ni kwamba hatuna imani wala dini..Dini yetu ni Ubinafsi na Mungu wetu ni Fedha..Tushauza roho zetu kwa shetani ili tupate Fedha, tunaua wenzetu ili tupate Fedha, tunadhulumu wenzetu ili tupate Fedha.. hatujali mwengine zaidi yetu na yote haya kwasababu ya KULEANA na KUOGOPANA..

Wednesday, 6 July 2011

My View on Investors and Investments

On paper foreign investments seems to be the right remedy for economic ills facing many poor countries. As many people have pointed out that foreign investors are supposed to provide opportunity for the host country to develop its natural and human resources, on contrary companies are profit driven with multitude of shareholders waiting for their invested bucks. Well established companies will seek any opportunity to increase their profit margin without care as long as their backers are happy. That’s why bigger companies have a wall of lawyers surrounding them in case of legal action against them.

Where do we stand?, as countries dependent on foreign donation to carryout basic functions of our governments we are between a rock and hard surface, we are bound to be squashed. Do we have to welcome foreign investors who are bent on exploitation? The answer in my view is NO. We as the owners of our own land and what is in it we have to have the final say on terms of which who ever is interested would abide and adhere to. We should be the one writing up rules and regulations and terms of their activities in our countries and not otherwise.

I have nothing against people of goodwill for our country because I believe that not all companies are purely exploitative some have good policies that allow growth in both the companies and their host area of influence in both environmental and personal growth. The most pressing issue is that we do not have policy makers with expertise in looking after our natural resources, most of them look at the end of the balance sheet paper to see how much they will be taking home without regard to the impact of that investment on the environment and the population. This is evident on many cases aforementioned by many critics and activist. We all do the blame game and I think we have become experts on it, what we need is action plan and implementation of those plans. We all know that the earth has finite resources let alone a country like ours at this moment of having natural wealth abundance we are beggars when our natural resources are depleted what will we become.

China is now booming in terms of a phenomenon economic growth such that it is financing the whole world including America and it is to do with them exploiting their natural resources at tremendous rate. But naturally growth boom time is followed by bust time because they will not be able to sustain that growth forever due to finite availability of natural resources that’s why they are expanding their tentacles to countries like ours hoping to sustain their growth by collecting our natural resources to fuel their fire.

Now instead of us be in a position to negotiate these deals for our greater benefit we are doing the opposite by having few people without regard to the well being of the populace, making decisions that will impact our very existence in the near future. We can not allow few people to decide the fate of our lives our children lives for few bucks without a hint of shame that are putting this country in danger of both social and economic collapse.

The days of exploitation will never end if we do not take effective actions against it. They need our natural resources we should be ones putting up prices not them as they have been doing over millennia. They exploited us because we could not do anything with our produces (cotton, and others) we did not have technologies or industries to process them, it is still the same story we have rare earth minerals but we do not have industries to transform them into components used in mobile phones or other consumer gadgets.

This is different era now education is not confined in one part of the world it is global the same to technologies are not confined in one part of the world so we should put special emphasis is developing internal technologies and learn and copy other people technologies so that we can exploit our own natural resources and develop our know-how and hence transform our lives for the better. We should come-out of our shells and realise that things do not just happen they are done and we are the people who should do it.

In nineties we had a lot of small scale businesses producing goods ranging from shoes to the making of car accessories, what we needed was to support them and be proud of our own products and the government to offer special help to develop such businesses so that they can improve the quality of their products. We still have such business in various aspects of industries ranging from furniture making to mineral explorations. They need help because they are the majority employers in our country. Since not everyone will be employed by the government these small businesses are the backbone of the real economy if given chance and help in terms of knowledge and capital they will become a formidable force against poverty in our country.

We can play politics all the time to amuse our unquenchable friends but when the natural resources are gone they will be gone forever.


Mungu Ibariki Nchi yetu na utuondoshee UBINAFSI kwenye nafsi zetu


Sunday, 3 July 2011

TUNAJENGA NYUMBA YA MAENDELEO ISIYO NA MSINGI

Nyumba imara huanza kwenye mipango (plan) maalum inayozingatia vipengele muhimu vitakavyotumiwa ili nyumba itakayojengwa ihimili purukushani za maisha ya kila siku ya mtumiaji wa jengo hilo. Na nyumba imara huanzwa kwa kujenga msingi ulio imara uliothibitika kuweza kubeba uzito wa kuta na paa la nyumba na vitu vitakavyokuwemo na watumiaji wa nyumba hiyo. Nyumba ninayozungumzia hapa ni mfumo mzima wa maisha ya mtanzania na mazingira yake. Wote tunajua kuwa ili tuweze kupata maendeleo ya kweli lazima tuweke msingi imara wa maendeleo hayo.

Maendeleo yako mengi tunaweza kuyapima kwa kutumia kigezo cha muda kama kuna tofauti kati ya muda uliopita na wasasa basi kuna maendeleo. Maendeleo yanaweza kuwa chanya ama hasi. Kama tofauti iliyopo ni bora kuliko tulipoanzia basi tuna maendeleo chanya na kama hali ya sasa ni mbaya zaidi ya iliyopita basi tuna maendeleo hasi ama tunapiga hatua za kurudi nyuma badala ya kwenda mbele.
Tanzania tunahitaji maendeleo katika Nyanja nyingi tofauti kuanzia nyumbani mpaka makazini. Ni lazima tuamshe fikra zetu kuelewa tulipo na wapi tungependa tuwepo. Naamini wote tunapenda kuishi maisha bora kama tunayoona kwenye TV zinazoonyesha vipindi vya nchi za n’gambo japo mimi nisingependa tuishi kama kopi ya maisha ya TV hizo kwasababu tuna mengi ambayo ni vyema kujivunia na utamaduni ni moja ya mambo muhimu kuyashikilia na kuyaendeleza kwa mtazamo wetu wenyewe badala ya kushurutishwa mabadiliko na wageni. Lakini wengi wetu hatuna muda hata wa dakika moja kufikiri kwanini tupo katika hali hii na tufanye nini kuibadilisha. Wengi wetu huamini maisha bora huja kwa ngekewa ama njia za mkato ambazo wengi wenu mnazijua.

Wengi wetu tumegubikwa na giza la UBINAFSI linalotufanya tusiweze kuona jukumu la mchango wetu na wenzetu katika kubadilisha jamii inayotuzunguka Giza la UBINAFSI huanzia nyumbani na kuhamia makazini na serikalini na kutanda nchi nzima. Ubinafsi unatufanya tusiweze kutoa nafasi kwa yeyote mwengine zaidi yetu.

Nikirudi kwenye misingi bora ya nyumba ya maendeleo lazima kwanza niweke wazi kuwa mipango (Planning) na vitendo(action) ndio chanzo cha mafanikio. Wengi wetu tna mipango mingi na serikali yetu ina mipango mingi lakini vitendo ni tatizo kubwa. Wengi wetu hupanga lakini mara nyingi hupangua na kuamua kutotekeleza mipango yetu. Na serikali yetu imepanga mambo mengi lakini utekelezaji wa mipango hiyo hakuna. Mipango imebaki kwenye makabati ya kuhifadhia nyaraka ikioga vumbi. Na hata hiyo ambayo inayotekelezwa basi utekelezaji wake ni asilimia chache inayoshabihiana na mipango ya awali.
Kwa hiyo tumekosa watendaji na pia tumekosa wahakikishaji wa vitendo hivyo. Tunasheria nyingi lakini ubabe ndio unaotawala maamuzi yetu. Na hii inaonekana zaidi katika serikali kufanya uwekezaji toka nje ndio sera namba moja. Tunatumia mali nyingi kuliko faida itakayopatikana kuwavutia watu wa nje waje kuwekeza kwenye nchi yetu wakati kama ni uchimbaji wa madini hata hayo makampuni makubwa yalianza kwa kuchimba kwa kutumia sururu na matoroli na wakajiendeleza kielimu na kimsingi mpaka wakaweza kununua mashine za kuchimbia na magari ya kusomba mawe. Sasa kwanini na sie tusianze huko kwa kuendeleza kampuni za ndani ya nchi ambazo tuna uhakika wa kuunda ajira ya ndani na pia kujenga teknolojia ya ndani ambayo itahakikisha kuwa ajira inakuwa na utaalamu unazidi na pia pato linabaki ndani ya nchi na hayo ndio maendeleo ya kweli. Kwa nini tunapenda kuwa na ustawi wa tawi kutoa maua bila ya shina na mizizi.

Na msisitizo ni kwamba si ukweli kuwa hakuna watekelezaji ila hawapewi nafasi na kizingiti kikubwa ni ubinafsi uliopo. Hatupeani nafasi ya kujikuza na hatuna upendo wa kweli chuki na ubinafsi ndivyo vinavyotawala nafsi zetu, tunapenda kuona wenzetu wakiwa na tabu hatupendi kuona jirani ana hali nzuri zaidi yetu tunapenda sie tuwe juu zaidi. Na kama watu wana sifa za ubinafsi na chuki hata serikali inakuwa na sifa hizo kwasababu serikali ni mkusanyiko wa watu. Kwa hiyo chuki na ubinafsi zinatawala katika maamuzi muhimu ya taifa. Mfano ni hivi karibuni ambapo viongozi wetu wanasema hadharani kama pesa iliyoamuliwa kurejeshwa kwa wananchi wa Tanzania haitapelekwa serikalini basi watazuia hao watakaopewa pesa kunufaisha wananchi..kauli hii inaonyesha chuki na ubinafsi uliopo. Badala ya kuwa hii ni ushindi kwa jamii (WIN WIN situation) imekuwa bora tukose sote.

Na sasa viongozi wanataka kuruhusu kampuni za kigeni kuchimba madini ya Uranium katika mbuga ya Selous, kampuni zitakazochimba zinategemea kupata dola milioni 200 kwa mwaka na kuigawia serikali dola milioni tano ambapo ni sawa na asilimia mbili na nusu ya mapato. Je asilimia mbili na nusu inatosha kudhibiti uharibifu wa mazingira utakao tokana na uchimbaji wa madini haya ya hatari. ni Kweli tunataka kuendeleza uchumi lakini tunapapatikia vijichenji wakati noti tunawaachia wageni wakizipeleka kwao huku tukibaki na mashimo na madhara kwa mazingira na kwa watu na wanyama wanaozunguka machimbo.

Tunapenda njia za mkato bila kazi ngumu tunataka mambo ambayo yameshatengenezwa (ready made) wakati tunajua kuwa nchi zilizoendelea hazikuendelea kwa njia ya mkato kwa nini sisi tuweke njia ya mkato mbele. Njia ya mkato ndio inayofanya majumba yakaporomoka na hivyo hivyo uchumi wa nchi kudorora na kudumaa na kuwaacha wananchi wakiwa katika hali mbaya.

Inaonekana kama kwamba viongozi wako katika haraka ya kumaliza malighafi tulizonazo kama vile hawatarajii nchi hii kuwepo baada ya miaka mingi inayokuja. Ni kama hawajaelewa kuwa malighafi ndio itakayofanya nchi kuwa na nafasi katika mataifa siku zijazo. Ni kama mfanyabiashara mwenye kuuza mali zake kwa bei ya chee haraka apate kuhama. Nchi yenye kuelewa misingi ya maendeleo kwa mfano Marekani ni nchi yenye mafuta mengi kuliko zote duniani lakini wao ndio wanunuzi wakuu wa mafuta kutoka nchi nje. Inaonyesha jinsi walivyo na mipango ya nchi yao kujikimu kimahitaji miaka mingi inayokuja.

Msingi bora wa maendeleo ni kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kila hatua ya kujenga nchi na kuleta mabadiliko ambayo yanatokana na mikono yao wenyewe. Na nyumba isiyo na msingi si imara na hatimaye huporomoka.

Monday, 27 June 2011

MTAZAMO WANGU KUHUSU AMANI NA TAHADHARI YA KIFIZIKIA KATIKA NCHI ZA AFRIKA.

Kama mwanafizikia katika masuala ya kiatomiki-asilia (quantum) nimeweza kutambua umuhimu wa amani katika mfumo wa viasili ambapo kuna sheria maalum za kifizikia ambazo hufuatwa. Sheria hizo huhakikisha kuna kuwa na msawazo-suluhishi (homogeneity) kati ya viasili hivyo. Utauliza kweli hayo mkuu? Jibu ni kweli kwasababu japo viasili havipendi kukaa pamoja (fermions) lakini kutokana hali halisi ya mazingira hufikia muafaka wa kuishi pamoja kwa amani hali ambayo hata sisi wanadamu ambao tumetengezwa kwa viasili hivyo tunakuwa katika mazingira ambayo hatuna chaguzi zaidi ya kuishi pamoja kwa amani japo tuna tofauti nyingi.
Kitu kinachotufanya tuishi pamoja ni uvumilivu kati yetu kwa kupuuza tofauti zetu na kuimarisha yale yanayotufanya tuwe kitu kimoja. Katika kuvumiliana ndipo tunapata AMANI lakini UVUMILIVU hutegemea mambo mengi hasa katika jamii yetu ni upatikanaji na ugawanywaji wa mahitaji muhimu ndio hupewa umuhimu mkuu. Kama viumbe wenye fikra tumegawa madaraka kwa kundi la wachache waweze kusimamia mambo hayo na kutuongoza katika kuendeleza hali zetu za maisha.
Uvumilivu ni kama mpira wa manati unapovutika huweza kufanya kazi iliyokusudiwa. Lakini UVUMILIVU unaweza kutafsiriwa kama WOGA katika hali Fulani kwani kama ni foleni basi nyuma ya Uvumilivu ni Woga na mbele yake ni Unyama. Kwa hiyo jamii yeyote lazima itazame kwa uangalifu mipaka ya AMANI inayotokana na uvumilivu. Nchi yetu inasifika kwa kuwa na amani inayotokana na uvumilivu wa hali nyingi hivyo kuifanya nchi yetu iwe ni yenye uvumilivu mkuu kati ya wanajamii na pia kuwa na hatari kuu mara mipaka ya uvumilivu huo ikivukwa.
Nchi yetu ina makabila zaidi ya mia moja na pia kuna wafuasi wa dini mbalimbali pia kuna watu wa rangi mbali mbali na pia upatikanaji wa mahitaji muhimu katika maisha pia yamegawanyika mara nyingi kufuata tofauti tulizonazo. Sitaki kunyoosha kidole kwa kabila, dini ama rangi yeyote lakini ukweli unabaki kuwa tofauti ya walionacho na wasionacho ni kubwa.
Hii inaonekana katika miji yetu mikubwa kuwa kuna tabaka la watu ambalo linaundwa na viongozi waliochaguliwa na wanajamii kuhakikisha kuna masawazo wa upatikanaji wa mahitaji muhimu lakini badala ya kutetea matakwa ya jamii wameelemea kutetea wazi wazi maslahi binafsi. Hali hii ni hatari kwa uwe mvutiko (strain) wa uvumilivu kwa maana ukivuta sana mpira wa manati hukatika na mara nyingi matokeo ni majeraha kwa mvutaji. Hapa nataka kusema kuwa ile simenti inayoshikilia amani inayotokana na uvumilivu inaanza kumemenyuka. Hata katika viasili mvutiko (strain) unapozidi basi hufumka kwa kishindo kikuu ili amani ije ipatikane tena (relaxation to ground state).
Kwa sisi binaadamu ina maana uvumilivu ukipotea jamii itaingia kwenye eneo la unyama ambapo maisha na mali za wanajamii zitapotea kabla ya miaka kupita na kupata suluhu ya kuvumiliana tena. Tumeona hali hii ikitokea kwenye nchi nyingi kama Rwanda na Burundi, Sudani na kwengineko lakini ishara zake zimeanza kujitokeza nchini kwetu, mfano ni mauaji wa watu waliokwenda kuvunja nyumba pale Tegeta, mauaji ya Tarime na kwengineko.
AMANI inayotokana na uvumilivu inatoweka kila siku zinavyopita kiasi sasa naweza kusema sasa tunaingia kwenye amani inayotokana na WOGA. Na cha hatari zaidi WOGA ni hali tete (unstable state) ambayo si vyema kukaa nayo maana WOGA ukitutoka tunarukia kwenye UNYAMA ambao matokeo yake ni mauaji ya halaiki na upotevu wa mali na kurudisha nyuma hatua zote zilizotifikisha tulipo. Tujifunze hali iliyopo LIBYA na kwengineko ambako walikuwa na amani inayotokana na WOGA leo wameushinda WOGA wao na nchi imetumbukia kwenye vita kufuta maendeleo yote waliyopiga.
Sitabiri balaa lakini kwa mwenye akili ya kusoma nyakati atatambua kuwa tunaelekea huko kwenye balaa hali tunajua taathira yake. Leo hii vyama vya siasa vimekusanya ushawishi mkubwa kwa wananchi ambao hali zao ni duni badala ya kuweka maslahi ya wananchi mbele wameweka maslahi yao binafsi mbele zaidi kiasi maisha ya mwananchi wa wakaida yamekuwa magumu mara nyingi zaidi ya miaka iliyopita. Uchaguzi unaokuja 2015 utakuwa ni mtihani mkuu wa AMANI tuliyonayo.
Leo hii Wazazi wanashindwa kulea watoto wao hivyo watoto omba omba wanazidi kuongezeka. Wazazi wanashindwa kusomesha watoto. Vitendo vya kihalifu vinazidi kuongezeka na hivi ndivyo vitakavyoondoa WOGA na kututumbukiza katika janga. Zamani wananchi hawakujua nini kinachoendelea lakini dunia ya leo yenye mitandao na njia nyingi za mawasiliani zimefumbuwa macho na masikio ya wengi na hivyo ni jukumu la viongozi wetu kujua kuwa matokeo huwa ni vitendo vilivyofanywa kabla (CAUSALITY).. ili tupate matokeo mema tubadilishe vitendo vyetu vya sasa na kutimiza majukumu yetu kwa faida ya TAIFA letu na Wananchi wetu. Hoja zenye kutetea wananchi zinaposhindwa bungeni kwa utashi wa siasa ujue ndio chachu ya kutokomeza WOGA uliopo na kulikurubisha taifa katika uvunjifu wa AMANI.
Ndimi Mdau Mwanafunzi

Friday, 24 June 2011

MTAZAMO WANGU KUHUSU MADA YA JOHN MASHAKA NA MAJIBU YA HASSAN

Baada ya kusoma makala zote mbili za Ndugu Mashaka na Hassan, naona niweke mtazamo wangu pia katika mada hii nyeti. Kihistoria nchi za magharibi na mashariki zimekuwa katika ushindani mkubwa wa kuboresha uchumi wa nchi zao. Na katika kuboresha uchumi MALIGHAFIndio kuchocheo kikuu katika kukuza viwanda na uzalishaji bidhaa ambazo pia zinahitaji soko la kuuziwa. Katika karne iliyopita makampuni mengi yaliyokuwa katika nchi za magharibi zilihamisha uzalishaji toka nchi zao na kuanzisha viwanda katika nchi za mashariki hasa CHINA kwasababu ya urahisi wa gharama za uzalishaji (cheap labour).
Hii ilileta ufunuo mpya kwenye nchi yenye kuhubiri UKOMUNISTI na ikaleta kubadilika kwa sera za uchumi za nchi na hivyo kujikurubisha hasa kwenye mfumo wa kibepari unaoendeshwa kinyonyaji. Maendeleo ya viwanda CHINA vimesababisha mfumuko wa tofauti kati ya walionacho na wasionacho ambao hauendani na sera zao za KIKOMUNISTI. Katika nchi yenye watu bilioni zaidi ya moja, ni wachache wenye utajiri wa ajabu kama mfano aliotoa ndugu Hassan na waliobaki ni masikini hata wengine ni masikini zaidi ya WAAFRIKA.
Swali linakuja KWANINI AFRIKA?...hapa ukweli ni kwamba si WACHINA tu wenye tamaa ya kujifaidisha kutokana na malighafi zilizoko katika bara la afrika hata hawa wa MAGHARIBI (marekani na nchi za ulaya) wamekuwa wakilitumia bara la AFRIKA kama shamba la BIBI toka enzi walipotambua kuwa kuna bara la AFRIKA.
JE WAAFRIKA TUFANYEJE? Hili ni swali ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza kwasababu mpaka jirani aje kukuomba chumvi ujue ameishiwa ama ana mipango ya kutumia yako ili yake imfae baadae. Kwa bahati mbaya kwetu ama nzuri kwao tumekuwa tukiongozwa na viongozi wenye upeo wenye urefu wa kope za macho yao kwa hiyo hawa majirani zetu kupitia mazingira ya kutusaidia wameweza kutupumbaza kiasi cha kutoona UTAJIRI TULIONAO. Tuchague viongozi wenye kuona shida zetu na kuzitafutia suluhu na pia wenye UZALENDO na upendo wa kuona wote tunafaidi keki ya TAIFA na pia kujali vizazi vyetu vijavyo na kuvilinda ili viweze kurithi mirathi bora.
Na ukosefu wa ELIMU umetufanya tusiweze kuona umuhimu wa kutumia na kulinda mali zetu kwa faida yetu hivyo tunakaribisha majirani walime wavune watuuzie mazao kwa bei wanayotaka wao. Si kwamba sipendi majirani lakini kama jirani macho yake ni kuninyonya kwasababu sijapata uwezo wa kutambua umuhimu wa nyumba yangu huyo si jirani mwema. Kwa ndugu Hassani ni kweli CHINA ilijenga viwanda na pia ikajenga TAZARA lakini ujue CHINA ya mwaka 70 si CHINA ya mwaka 2011. Na Pia NCHI za magharibi ni zile zile zilizotunyonya na mpaka sasa zinaendelea kutunyonya bila kujali huku wakitupachika jina la UMASIKINI wakati utajiri wao unatokana na MALIGHAFI ZETU.
WAAFRIKA tunahitaji viongozi wenye UZALENDO wa nchi zao wenye kujua umuhimu wa wananchi wao ili kama ni kufaidi matunda ya nchi basi tufaidi sote badala ya kujigawia kijambazi mali za MATAIFA yetu kwa kisingizio cha uwekezaji wakati mikataba ya UWEKEZAJI huo yanafaidisha upande mmoja. Lazima viongozi wetu wawe na NGUVU ya kusema kuwa kama unataka kuwekeza NGUVU KAZI lazima iwe ya humu ndani hatutaki uwekezaji ambao ni uhamishaji wa watu toka CHINA ama MAGHARIBI kuja kufanya kazi ambazo wenyeji wanaweza kufanya na kama unahitaji wataaluma basi chukua wazalendo wapewe mafunzo wawe wataaluma.
LAZIMA tuamke na kujua malighafi zina idadi maalum zikiisha tutafanya nini wakati hatufaidiki nazo wakati zipo...VIONGOZI WETU MTUONEE HURUMA NA KUTAMBUA HALI ZETU NA KUHAKIKISHA MIPANGO MAALUMU ILI NCHI YETU IWEPO PIA BAADA YA MIAKA ELFU..
kwa hiyo nahitimiza mtazamo wangu kuwa kabla hatujawanyooshea vidole WACHINA na WAZUNGU tujiangalie sisi binafsi tuna upendo gani kwa nchi yetu na wananchi wetu. Na Tusiogope kuwaambia VIONGOZI wetu kuwa sisi wananchi ndio tunaoweza kuleta maendeleo ya nchi kama TUKIWEZESHWA na TUKAJIWEZESHA na pia tuwaambie usoni bila haya ama kuogopa kuwa UMASIKINI tulionao ni wakujitakia na wao tumewachagua kwa sifa ili watukomboe na sio kutuangamiza. Washughulikie SERA za maendeleo wafukuze wala rushwa na wabadhirifu wa MALI za umma na WASIUZE nchi yetu kwa BEI ya kujinufaisha wao binafsi....
Mdau Mwanafunzi..

Friday, 10 June 2011

UWELEWA WA UTAJIRI WA MAZINGIRA NA MAENDELEO YA MWANADAMU

Kwanza kabisa nianze kwa kusema kuwa Mwenyezi Mungu ametubariki kwa utajiri wa maliasili uliotukuka katika nchi yetu ya Tanzania. Tukianzia kwenye Bahari na mpaka Maziwa. Ni nchi pekee katika bara la afrika kuzungukwa na maziwa makuu matatu. Yenye uoto wa asili na ndipo panaposadikiwa kuwa mpaka sasa inasadikika kuwa binaadamu wa kwanza alitoka hapa kutokana na rekodi za fuvu lililovumbuliwa kule Olduvai Gorge. Tuna mbuga nyingi lakini katika mbuga hizo Serengeti ndio kinara wa mbuga zote duniani kwa kuwa na mkusanyiko mkubwa wa wanyama katika eneo moja.
Tokea enzi za zama uhusiano wa binaadamu na mazingira yake umekuwa ndio chachu ya maendeleo yake. Kutokana na uwezo wetu wa kufikiri tumeweza kuyafanya mazingira yetu kuwa nguzo kuu ya utegemezi na ni mhimili wa kuwepo kwetu. Mara zote tumeweza kuchukua kila kinachotoka kwenye mazingira yetu kwa faida yetu bila kujali athari kwasababu tunaona dunia ni kubwa hivyo athari zetu ni kidogo. Wengi wetu tunaamini kuwa dunia ina malighafi isiyokwisha (infinite resource) lakini ukweli ni kwamba kuna idadi maalum ya malighafi iliyopo duniani hivyo tunapotumia ikiisha tufahamu kuwa vizazi vinavyokuja vitasumbuka kwa kurithi deni la malighafi ambalo hawataweza kulipa na hivyo kwa wenye kujua hesabu kuna kitu kinaitwa mapato yenye kupungua (diminishing returns).
Hii imetokea kwenye miji mingi ya kizamani ambapo wakaazi walitumia malighafi zao kwa fujo na baada ya kuisha na wao maisha yao yakawa hatarini hivyo wenye uwezo walihama kwenda sehemu nyengine na wasiojiweza wakaishia kupoteza maisha. Leo hii nchi zimewekwa mipaka hivyo kuhama si suala la kufikirika. Ndio maana wamarekani wanafikiria kuhamia kwenye sayari nyengine ili wapate malighafi toka huko. Na kugombea malighafi ndio chanzo cha vita vyote kuanzia wanafamilia mpaka nchi na nchi nyengine.
Sasa tuangalie katika nchi yetu na malighafi tulizonazo na nini tunafanya. Tumewapa wawekezaji panga wajikatie mapande wanayotaka ili mradi watupe asilimia chache za mapato na kuwapa msamaha wa kodi. Upande wa madini tunawaachia wakivuna dhahabu tani kwa tani bila kufahamu dhahabu huisha na zikiisha na wawekezaji nao watahama kurejea kwao na sie tutabaki na simulizi za mashimo matupu na taathira za mazingira tutakazobaki nazo miaka mingi inayokuja kutokana na kemikali za sumu zinazotumika kuchimbia dhahabu hizo. Vizazi vijavyo watapata simulizi tu jinsi tulivyokuwa matajiri bila kuona faida ya utajiri huo (Lodi Lofa).
Wenzetu wanafikiria watakuwa wapi baada ya miaka mia tatu ijayo na kufanya kila aina ya hesabu kujua hatma yao kutokana na mahitaji ya jamii na malighafi zilizopo, sie tunajali ya leo tu tukishapewa ten percent tunauza urithi ili mradi tupate kuendesha Hummer na Lexus. Tunaangalia idadi ya watanzania kama ni tatizo badala ya kuwa ndio jawabu la matatizo mengi tunayongojea wageni watusaidie. Ukweli ni kwamba hakuna msaada wa bure siku zote ni “nipe nikupe”, hii ndio inayovutia nchi nyengine kuwekeza kwenye nchi ngeni ili waweze kujaliza mapungufu yao. Na kama huna mipango maalum ya kudhibiti matumizi ya malighafi yako ndio unakuwa kivutio kikuu.
Nchi nyingi za Afrika zimekuwa ndio waongozaji wa kutoa malighafi na pia kugeuzwa soko la bidhaa zinazotokana na malighafi hizo. Kiasi ni biashara yenye kulipa sana kwasababu nanunua malighafi kwa shilingi moja natengeza kitu nakuuzia shilingi kumi.. halafu unashangaa kwanini deni la taifa linazidi kila dakika inayopita.
Suluhisho ni kuweka kipaumbele elimu zote na kuweka umuhimu zaidi katika ufundi uhandisi(engineering) ili tutengeneze viwanda ili sisi wenyewe tutumie malighafi zetu na pia kupata ajira za uhakika tutengeneze bidhaa tuuzie wananchi wetu hivyo kuinua hali ya maisha yetu tujiendeleze wenyewe kisayansi na kiteknolojia badala ya kutegemea bidhaa zilizokwisha tengenezwa (finished products). Najua wengi mtapinga kutokana na nadharia ya kupata pesa chap chap lakini pesa unazopata bila mpango hupotea pia bila mpango. Na wenye fikra walisema kama hupangi mipango ya kufaulu basi mipango ya kufeli hujipanga yenyewe.
Na tuanzishe mipango maalum ya kuwavutia watoto wetu katika kuelewa na kuheshimu mila na itikadi zetu na mazingira tunayoishi ikiwamo miti na wanyama waliomo kwasababu tumezaliwa katika nchi hii kwa sababu maalum. Basi na tujue jukumu letu katika hayo kwasababu wazee wetu hawakupigana kufa kupona ili tuwe huru halafu turudi tena kwenye utumwa wa kileo. Na hayo ninayosema yanawezekana kwasababu nchi kama Malaysia miaka 30 iliyopita ilikuwa maskini leo hii ni moja ya nchi tajiri kutoka na mikakati ya kujiendeleza waliyoweka. Leo hii wamekumbatia Sayansi na Teknolojia ya kweli kiasi wengi wenu mnapeleka huko watoto kusoma. Basi nasi tufumbue macho tuweze kuona...
Mungu Ibariki Tanzania, na Utupe ufunuo na Upendo kwenye fikra zetu.
Mdau Mwanafunzi.

Tuesday, 7 June 2011

Jawabu la kauli ya Madaraka kuhusu Ujenzi wa barabara katika Mbuga ya Serengeti.





Baada ya kusoma kauli mada iliyotolewa na Ndugu Madaraka Nyerere kuhusu ujenzi wa barabara katika mbuga ya kuhifadhia wanyama ya Serengeti nimeona na mie niseme jambo.
Kwanza kabisa nianze kwa kusema nimesikitishwa na mawazo ya Ndugu Madaraka kuhusu katika kufananisha athari ya ujenzi wa barabara na mapito ya wanyama hao katika maeneo yenye wanyama wakali kama simba na mito iliyojaa mamba. Amesahau kuwa kuwepo kwa wanyama wanaokula wanyama wenzao (Predators) ni msawazo maalum katika mizani ya maisha ya wanyama hao. Wenye kula majani wanategemea wanyama wanaowinda katika kuhakikisha kuwa idadi yao inahimili mazingira waliyopo. Na pia Simba na wanyama wawindaji huchunguza kundi kabla ya kuwinda wakiona mwenye matatizo (weak) ndio wanamuwinda hivyo kuacha wenye afya njema wakiendelea.
Athari ya barabara katika mbuga sio tu kwamba itabomoa natural order ya wanyama hao bali itabadili mazingira, je umefikiria suala la uchafuzi wa mazingira utakaotokana na gesi chafu za magari (air pollution) na kemikali zitakazomwagika kama mafuta ya magari, sauti za magari(sound pollution), uchafu utakaotupwa ovyo na wapiti njia, idadi ya wanyama watakakufa kwa kugongwa na magari, njia rahisi kwa majangili kuuwa wanyama hao, idadi ya askari pori watakaohitajika kulinda wezi wa nyara, uharibifu wa mioto asilia na kujenga mipaka isiyo asilia. Hayo ni kwa upande wetu na jinsi gani wanyama watakavyopokea kuwepo kwa barabara na mambo yatakayoletwa na hiyo barabara.
Tumekuwa masikini katika upande wa kuelewa mazingira yetu kiasi leo ni wageni wenye utaalamu katika kuelezea maisha na tabia za wanyama wanaoishi kwenye mbuga zetu kiasi sisi tumebaki wabeba vifaa ya kupigia picha na wapelekaji wa watu porini.
Tumeshindwa kufahamu tabia za wanyama na faida zao kiasi tunawaona kama kikwazo kwetu badala ya kuwa ni tija yenye thamani kuu. Leo hii tukimuona mbwa tunaokota jiwe kumpiga bila sababu wala fikra wakati mbwa huyo anaweza kutumika kutambua magonjwa kama Cancer katika mwili wa binadamu, ama kutambua kuwepo kwa dawa za kulevya ama silaha.
Leo hii wanasayansi wanamsoma Inzi kutambua uwezo wake wa ajabu wa kuweza kuruka na kutua katika dari ili waweze kuigiza katika mifumo ya kuendesha ndege lakini kwangu wewe na mimi tunamuona si kitu. Leo hii wanasayansi wanamsoma mjusi kutambua uwezo wake wa kutembea kwenye kuta na glasi ili waweze kutengeza gundi lakini kwangu mie na wewe tunaona bora tumpige fagio afe. Leo hii wataalamu wanatambua kwanini Simba dume halei watoto wa kambo kwangu mimi na wewe hii ni hadithi.
Leo hii tunachoona ni barabara tu bila kufikiri kuwa barabara si lami tu ilotandazwa bali ni mfumo mzima wenye taathira kuu kila inapopita. Kuhifadhi mazingira ni jukumu la taifa zima na kuwepo kwa mbuga iwe ni chachu ya kutambua umuhimu wake kuwepo pale.
Leo hii wanyama kama Simba wameingizwa kwenye Listi ya wanyama watakaopotea baada ya miaka michache inayokuja kutokana na shughuli za binaadamu kuhamia katika mazingira yao hivyo kuzuia mihamo yao kutoka katika familia walizozaliwa kwenda kuhamia kwenye familia nyengine ili kuepusha kuzaliana wenyewe kwa wenyewe na hiyo kusababisha madhara ya uzaofinyu (Inbreeding). Kwa hili hata sisi binadamu tunaweza kujifunza lakini kwasababu ya umasikini wa fikra hatulioni hili.
Suala la kusema mahitaji ya wanyama yamewekwa mbele zaidi ya binadamu kwanza tukumbuke kuwa binadamu ni mnyama pia. Na katika mfumo mzima wa maisha wanyama wote wana mchango maalumu katika kuwepo kwao. Kutokana na ubinafsi wa binadamu na kujifanya kuwa na akili nyingi tumeharibu sehemu nyingi za mfumo huu kiasi taathira zake zimekuwa zikituangamiza sisi wenyewe.
Tanzania tumebarikiwa kuwa na utajiri asilia ambao ni bora kuliko faida ya hiyo barabara. Tunachotakiwa ni kufahamu utajiri huo na kuuthamanisha ili tuweze kupata tija. Wenzetu wa nje sio kwamba wanatukwaza bali kutokana na ukosefu wa elimu na kutoona mbali tulionao wanatuonea huruma tukija kupoteza utajiri huu tutakwenda kwa nani.
Wazungu waliwaua wanyama wenye kuwinda na kuwindwa kwenye nchi zao baada ya miaka mia ndio wakaona taathira waliyofanya na sasa wanatumia mabilioni ya pesa kurudisha wanyama hao ili wabalance ile natural order iliokuwepo. Leo hii kwenda kutazama ndege kipanga inabidi uombe leseni na hupati leseni hiyo bure ni lazima watizame historia yako, sie kwetu bure tunawaona wasumbufu wanaotuibia kuku. Dar es salaam kulikuwa na ndege kila aina miaka ya tisini leo hii waliobaki ni kunguru je unaijua sababu?
Watanzania tuache maneno ya kisiasa penye kuhitajika utaalamu..inaonyesha tuko tayari kuuza shamba kwa mlo wa leo tu..
Mungu Ibariki Tanzania na Tupe ufunuo katika fikra zetu.
Mdau Mwanafunzi.

Friday, 27 May 2011

Barua Yangu Kwa Raisi

Mheshimiwa Baba Raisi wa nchi yangu,

Ni mimi mwanao Shida na ndugu yangu Tabu, tumeona leo tuandike barua kwako ili uweze kukumbuka hali zetu. Sisi tuwazima japo wiki iliyopita Malaria na Kipindupindu kilitaka kutuhamisha duniani. Natumai nawe umzima wa afya na uko katika pirika pirika za kutuletea unafuu wa maisha.


Juzi nilimuona Mjomba WAZIRI akipita na gari lake lenye vioo vyeusi njiani wakati natoka kumtazama bibi majuto. Pengine kutokana na weusi wa vioo na jua lilikuwa likituchoma hakuweza kutuona na hivyo tulichoambulia ni vumbi.

Nakukumbusha kuwa huku kwetu jua bado linawaka kwenye mifuko ya suruali ya kila ninayepishana nae njiani. Kwa hiyo naomba utuangazie macho nasi tupate kuona maana njaa inazidi kutukosesha amani. Vijana wamejiajiri kukosha magari ya wapitao lakini wengine wanaouza mahindi na maji purukushani na Mgambo haziishi.

Sina imani tena kila nikimuona polisi nakimbia badala ya kumsogelea ili anilinde kwasababu majuzi Tabu aliwekewa kipande cha bangi mfukoni na kuambiwa ni mzururaji pia. Mimi nimechoka kuomba omba njiani kila nikijiajiri naona watumishi wako wananijengea vizingiti nishindwe kupita. Kwa hiyo nakuomba utupunguzie matatizo yaliyo ndani ya uwezo wako na natumai unayajua maana yalikuwa katika zile ahadi ulizotoa wakati wa uchaguzi..


Ndimi Shida na ndugu yangu Tabu

Tuesday, 24 May 2011

Ukweli na Uwazi ni Bidhaa Adimu Afrika

Ukweli na Uwazi ni bidhaa adimu mno kwenye nchi za Afrika..Ukweli na Uwazi ni adimu katika serikali, na adimu kwa wanasiasa, hata katika familia nyingi za kiafrika ni adimu kupindukia..

Ukweli na Uwazi ni adimu hata kati ya Mke na Mume, kati ya Watoto na wazazi wao, kati ya Marafiki, Kati ya ndugu. Ukweli na Uwazi ni bidhaa adimu lakini inauzwa kwa bei rahisi ajabu...
BEI YAKE NI BUREEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEEE

Thursday, 19 May 2011

Ulafi wa Viongozi wa Nchi Afrika na Hand-off Approach



Nchi nyingi za Afrika ziko mikononi mwa serikali ambazo zinaongozwa na watu wasio na chembe ya huruma kwa umma wanaoongoza. Wengi wao ni urithi tulioachiwa na wakoloni kwa hiyo dhamira zao hazijabadilika toka kuwa watumishi wa kikoloni kunyonya wananchi wenzao mpaka wakawa wenye uchungu na nchi na kujivika taji la uzalendo.






Uzalendo ni kitu adimu katika serikali hizi japo majukwaani huhubiri uzalendo utadhani uzalendo ni nguo unayoweza kuifua na kuivaa. Uzalendo uko moyoni, uzalendo ni sumu ya unyonyaji, uzalendo ni sumu ya rushwa, uzalendo ni sumu ya ukandamizaji, uzalendo ni sumu ya uonevu, uzalendo ni dawa kwa wananchi.



Uzalendo ni chachu ya ukombozi na uzalendo ni chocheo ya maendeleo ya nchi
Uzalendo huleta upendo katika nchi huleta neema huleta amani huleta furaha ya nchi
.


Leo hii viongozi wameamua kujivua majukumu ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa sawa katika kushiriki masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Eti ni jukumu la wananchi kuleta maendeleo wakati wao wanazidisha kujenga vipingamizi vya maendeleo hayo. Mwananchi akifanya biashara badala ya kusaidiwa kielimu na kifedha ili aweze kuendelea, itafanywa kila mbinu ili asifikie lengo na mwisho kukata tamaa.






Pesa za kodi zinaishia kujenga mahekalu na kununua magari ya kifahari ya viongozi wakati wananchi nyumba zao za udongo zilizoezekwa nyasi. Shule hazina viti vya kukalia wala walimu wa kutosha, hospitali hakuna vitanda wagonjwa wanalala chini na hakuna dawa za kutosha wala madaktari wa kutoa huduma..Eti kiongozi mzima anasema nendeni LOLIONDO MTAPONA!!!!

Tuesday, 17 May 2011

Usafiri wa Mbagala Kilakshari

Nimeona niitafsiri hii maana kila nikiisoma nacheka mbavu sina:
Utakuwa mshamba kama hujawahi kupanda daladala aina ya DCM toka kigamboni kwenda Mbagala rangi tatu! Kweli we utakuwa unatoka dunia nyengine kabisaaa!! Hujafika BONGO kwa nini usikatae na kuniona mie muongo ili ukapande daladala toka Feri kwenda Mbagala au Feri Mwenge au Kariakoo kuelekea Bunju. Basi siku moja nikaamua kwenda kutembea Mbagala kupitia feri kuzurura si unajua Utalii sio mpaka uende Manyara, Selous ama Serengeti.. Tripu nzima ni Buku mbili na pesa ya juisi na mihogo ya kuchoma.

Basi nikapanda daladala DCM limechoka na limejaa ile mbaya huku moshi umezingira basi zima. siku hesabu lakini tulikuwa kama watu 80 kwenye basi la abiria 40. Hapa ndio BONGO, wasafiri wengine wanapanda kupitia madirishani wengine mlangoni basi ili mradi usivae shati jeupe utafika unakokwenda likiwa jeusi kwa magirisi na shombo za samaki. lakini hii si ajabu kwa wakazi wa Mbagala washazoea.. Wengine wanakula vipande vya miwa, kuna wakinamama na mabeseni yao ya samaki, wengi wao ni samaki aina ya chuchunge, Msimu wa chuchunge babu...wengine wanakula machungwa na wapitisha pweza madirishani wanauza juu kwa juu.
"Lete Pwezaa bwana dawa ya chakula cha usiku hao"...
Kuna jamaa wanavuta sigara na hakuna anayethubutu kusema Neno..Sema kitu uishie kulazwa muhimbili na majeraha ya kichwa na pengine upate tetnus ukipona we unabahati.
Basi lilijaa lakini Konda kakazana kusukuma watu wajae zaidi huku akitangaza

"KUNA NAFASI ZA KULALA !!! SITI KIBAAAAAOOO, GARI HAIJAI INAJAA NDOO YA MAJI!!!"

Kuna jamaa wako juu ya gari washalipa nauli kabla ya kuruhusiwa kupanda ngazi kuelekea mbinguni..Baada ya dreva kuridhika kwamba mlango haufungiki kwa watu kujaa tukaanza safari ndani la gari la maraha kuelekea MBAGALAAAAAA!!!.
Basi linanuka moshi wa sigara, Pombe, samaki na moshi mchafu wa gari..watu wakaanza maneno kama ndege kwenye tawi la muwembe.

"We dada uwe unanyoa j amani !!! Mrembo mzuri lakini kikwapa kinanuka!!!" "Mpashe huyooo...kasuka nywele utazania kalambwa na ng'ombe!!! Eti ndio katoa shilingi alfu saluni! mie kama ni mke wangu namnyoa usiku...zooote akiamka kama kibwengo!!"

"Mrembo gani huyu hebu mwone midomo kama subiani...hivi anajiona kapendeza sanaaaa!!! Eti wanaiga wazungu lipustiki!!!" " Kama ni mke wangu wallah nakuapia talaka saba!!! Ati anajifanya misstanzania ...kumbe kalalia mlo wa mhogo na mchicha!!!"

Nikajua hapa kitanuka sasa hivi kuna chungu kinapikwa. Kuna mzee wa makamo kwenye siti ya nyuma akaanza kutapika, harufu balaaa..

"Eheee!!! gongo la kigamboni hilo !!!." Kwani Kigamboni kuna gongo la bure??? Pesa yangu nakula...nitakutoa nishai... Wee kama huna hela shauri lako macho kama kenge kasoro mkia etcetc.

sie wengine tukanyamaza kimya kama hatujasikia kitu tusije tukajeruhiwa kwa kosa la mropokaji.
mara kidogo:

We mama mbona unanikalia? na minguo yako imelowa misamaki???unajua bei ya hii suruali yangu?? Umewahi kukaliwa weee,koma kabisa!!! kama una ubavu si ushuke ukapande taxi??? Wee mama si ungepanda ungo,mwanga mkubwa wee!!!

matusi yakazidi kuporomoshwa tukajikuta kituo cha polisi cha Kilwa Road Sio kwa ajili ya matusi bali Konda ambae anaonekana kakimbia umande zamani kuna jamaa anajidai kalala hataki kulipa nauli. konda kumuamsha alipe nauli ikawa kosa. Mwanaharamu jicho jekundu kwa Bangi na harufu nzito ya Gongo la kigamboni kaja juu.

"SILIPI NAULI sina SHILINGI NA UNAWEZA KWENDA POPOTE"

..KONDA akamuacha akakusanya nauli kwa waliotaka kulipa halafu akamrejea jamaa wenye jicho kama shetani. Konda miraba minne akamkunja jamaa huku akidai nauli...Ohhooo Jamaa kachomoa kisu na Konda katoa BISIBISI, wengine tunaangukiana tukijiepusha tusijechomwa na bisibisi ama kisu..
DEREVA peleka gari polisi kuna chizi hataki kulipa nauli halafu ana kisu lazima aende selo huyu..
Bahati tulikuwa karibu na kituo cha polisi Kilwa Road. Ikabidi dereva apeleke daladala lilijaa kupita kiasi kituoni.. Kuna jamaa akasema
"hivi kweli abiria tunapelekwa polisi kwa ajili ya shilingi mia mbili tu?? Mimi nitamlipia!"
lakini basi lilishaingia kituoni. Kuna afande akaja kuuliza kulikoni.. "Afande kulikuwa na Chizi hataki kulipa lakini mimi nitamlipia!
"HEE MMEKUJA KWENYE MAONYESHO YA FASHION HAPA KITUONI..SHUKENI MMOJA MMOJA TOKENI HARAKA.. WE DREVA NENDA KAANDIKE RIPOTI KULE NDANI"
Yule afande akakaripia..
"Mmekuja kuuza sura hapa? gari imejaa kama ile ya Mererani, nanyi abiria mnakubali kupangwa kama sangara!!!Halafu unadhani utaondoka hivi hivi tu hapa? Gari yako kwanza ni mbovu na hii ni wiki ya usalama haijakaguliwa hii!!!"
Yule jamaa aliyetapika hakushuka akaachwa anakoroma ndani ya daladala.. Baada ya saa nzima na bonge la tabasamu la wale afande tukaruhusiwa sikujua nini kilichowafurahisha kiasi cha kutuaga "MWENDE SALAMA"..HIVI yale mabasi ya KASI yakowapi ama nilikuwa ndotoni tu???

Ni lini serikali za Afrika zitatumia wasomi katika Maamuzi

Imekuwa ni desturi kwa serikali za nchi nyingi za Afrika kufanya maamuzi makubwa yahusuyo Uchumi,Afya,na maendeleo Jamii kisiasa. Kama nikikumbuka vyema Siasa ni muhimu katika jamii lakini mchango wake lazima uwe unategemea Elimu iliyothibitika. Katika dunia ya sasa ya Utandawazi ama globalisation nchi isiyofanya jitihada maalumu za kujikwamua kwa kutumia michango ya elimu mbali mbali ambazo zimo ndani na nje ya nchi zitajikuta zikiyumba na mwisho wake amani na imani waliyonayo wananchi itatoweka pia.

Nchi za Magharibi zinafanya kila jitihada kuhakikisha wananchi wake wanapata mahitaji yao ya msingi kwa gharama nafuu na kwa ubora wa hali ya juu..cha kusikitisha nchi nyingi za kiafrika ikiwemo Tanzania zimejivua jukumu hilo na kuwa na kila mtu ale kwa urefu wa mikono yake ama Hands-off approach. Majukwaani wanahubiri ya Musa vitendoni wanatenda ya Firauni.

Mambo muhimu kama uboreshaji wa huduma za afya na elimu zinasubiri wahisani na misaada yao wakati kodi inatumika kulipa mishahara na marupurupu ya waendeshaji serikali wakiwemo wabunge ambayo iko juu zaidi ya mawingu tena bila woga wala haya juu ya wananchi wenziwao ambao ni masikini hata kujua watakula nini kesho ni ukuta.

Itakuwa sawa kwamba wasomi ni adui wakubwa wa serikali za kiafrika ndio maana wengi wao wamekimbia nchi zao na kunufaisha nchi za magharibi na kwengineko.Rafiki yangu mmoja alinambia hatutaki wasomi bakini huko huko. Ukiwa na mwerevu katika kundi la wajinga basi wewe ndio utakuwa mjinga na wao ndio werevu kwasababu wingi ni nguvu hata kama ni ujinga.

Wednesday, 12 January 2011

Kilimo kwanza na sera za vichwa maji


Jana nilibahatika kumsikiliza Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania alipotembelea London. Katika Mazungumzo yake moja ya ujio wake ilikuwa kumuaga aliyekuwa balozi hapa London Bi Maajar. Pia aligusia mipango ya serikali katika jitihada za kuleta maendeleo ya nchi kupitia KILIMO.

Nilifurahi kuona Mheshimiwa anaelewa vyema kuwa JEMBE la mkono halitotufikisha mbali. Suala ni njia gani zitumike ili mabadiliko ya kweli ya kilimo yatokee... Hili ni suala zito kwa maana inahitaji mipango madhubuti itakayoshirikisha wadau na wana sayansi wa kilimo na sayansi nyenginezo ili kuleta jawabu litakalofaa kusukuma gurudumu hili zito. Tatizo lililopo Waafrika kwa ujumla tumekosa MWAMKO (PASSION) ya kufanya jambo likafanikiwa.

Tumebweteka na kutaka matokeo ya kazi yaonekane hapo hapo kwa ujumla tumekosa subira. Na hili limetufanya tuogope kufanya miradi ya muda mrefu. Tumeweka ujira mbele kuliko ajira yenyewe. Tunataka malipo kabla hata biashara haijauzwa. Na kwa mtazamo huu hatufiki popote.

Serikali hata ikawa na mipango thabiti ya kutokomeza umasikini kama hakuna watekelezaji wa mipango hiyo itakuwa ni kama hadithi isiyokwisha. Passion ndio ilofanya watu wakagundua Umeme. Passion ndio ilofanya watu wakagundua Machine. Passion ndio siri ya maendeleo ya nchi za magharibi.

Kuna watu wanatumia maisha yao yote kuchunguza kitu kimoja mpaka waone mwisho wake. Na mara nyingi jitihada hizo hulipa na kuleta mabadiliko makubwa katika jamii wanazoishi. Na malipo yao ni zaidi ya pesa, Hutajwa na hawatosahaulika mpaka mwisho wa dunia kutokana na michango yao. JEE SISI TUNAWEZA HAYO...? Jibu tunaweza ila inabidi tubadilike ila je wangapi wanapenda mabadiliko? Jibu ni wachache tushazoea maisha ya kuzugazuga. WASEMAJI GUNIA WATEKELEZAJI PUNJE...

Saturday, 8 January 2011

Narudi Shambani na Jembe Langu

Miaka imepita tangu nitume new post, mambo mengi masomo, maisha, matatizo na nakadhalika!! anyway napenda kuwakumbusha wadanganyika na wadanganyifu kuwa badala ya kugombania fupa kuna n'gombe mzima anahitaji kuliwa..

Wednesday, 7 October 2009

My Vision for Tanzania

My Vision for Tanzania

For a while I have been wondering why the political situation in Tanzania has become a major headache for all citizens especially during the election times. Since the introduction of multiparty system in 1990s, the country has seen major divisions instead of national unity. The population have been politicised in such a way that one is pitted against another, husband against the wife, families against family members, tribe against tribesmen and so on.

Politicians have turned population into dogmatic followers. Politics has become new religion where switching is seen as fit for mob lynching. Instead of supporting a party for their policies, the population has been divided into them against us. No matter what kinds of policies are put forward by the leaders of the parties, the followers are forced to support and defend them even if they are idiotic policies rendered to discriminate the masses as opposing is forbidden fallacy.

My mum support CCM and my dad support CUF and I could see how their affiliation to their political parties affect their own relation as a wife and husband. The arguments that erupt frequently put the family equation on the balance. I know who to blame and may be suggest an alternative solution to our domestic and society problem which is politics.

From my experience of living in Europe, I have observed that the politics in only for the few and their relation to the populace are their projected policies which are extensively debated to see who has better deal for the people. We should learn from those who are best according to those who have knowledge. The European politicians put down figures for example the party will put in their manifest that for health they will improve it by introducing such and such measures and they will fund the measures using such and such money which they will get from such and such sources. That information is then verified to see whether it will be feasible and their effect to the population. The other parties will also pitch their policies on the same and then it is up to the masses to decide who they should vote for according to their policies and not because of their affiliation to such political party. That’s why there are no political backlashes after elections and that is why the leaders may even concede before all votes are counted and such is what is lacking in Tanzania and the rest of African countries.

For us to come out of this vicious circle of heavily politicised population where you have government servants and government apparati working according to their political affiliations, we need to start DEPOLITICISING the masses before it is too late and before another batch of people lose their lives and others are injured for life because of politics while the leaders of the political parties toss a drink together.

Wednesday, 2 September 2009

UMASIKINI AFRIKA-NI WAPI NDOTO ZA MATUNDA YA UHURU ZILIPOGEUKA JINAMIZI

Ukitazama historia ya nchi nyingi za afrika wakati wa kupigania uhuru toka kwa wakoloni utagundua kuwa japo ilikuwa lazima mwafrika awe huru lakini wapigania uhuru hawakuwa na mipango madhubuti ya kuendesha nchi zao baada ya kupata uhuru huo. Miaka ya sitini ndio ilikuwa kipindi cha mabadiliko sehemu nyingi duniani zikiwemo nchi za magharibi. Kipindi hicho mabadiliko ya mtazamo wa jamii kuhusu maisha hasa katika nchi za magharibi ulikuwa chachu kwa nchi zilizokuwa chini ya wakoloni kujikomboa.

Kutokana na ukweli kwamba wazungu wasingeweza kuendelea kushikilia makoloni yao kutokana na harakati za kipindi hicho hawakuwa na budi kutoa uhuru kwa nchi walizokuwa wakizishikilia kama makoloni. Ulazima wa kutoa uhuru na ulazima wa kuendelea kunyonya makoloni hayo ulisababisha maamuzi magumu kufanyika. Na hapo ndipo mwanya wa kuchukua baadhi ya hao wagombea uhuru na kuwasomesha katika vyuo vikuu vyao ili kuwaandaa kuchukua hatamu za nchi zao. Ni ukweli usiopingika kuwa wagombea uhuru hao walikuwa na ndoto njema juu ya mafanikio yatakayopatikana baada ya kupata uhuru. Wananchi waliokuwa na matumaini ya kupata maisha bora zaidi ya waliyokuwa nayo kabla ya uhuru walitoa nguvu zao zote kufanikisha azma ya kuwa huru.

Tukitazama jinsi ya wakoloni walivyoweza kutawala tunaona jinsi walivyoweka mipango bora iliyosukwa rasmi katika kufanikisha unyonyaji wa mali toka kwenye makoloni hayo. Ukianzia ulinzi, ambapo ni jambo la muhimu sana katika unyonyaji, wakoloni waliweza kuweka majeshi ya polisi yaliyofunzwa mafunzo maalum ya kutia woga na hofu kwa wananchi ili wasiweze kuvuruga amani na kusababisha shughuli za unyonyaji kusimama. Pia waliweza kujenga njia za usafiri zilizowezesha kusafirisha mali kwa urahisi. Waliweka mfumo mzima ambao kwa kutumia njia ya “kuwagawa ili uwatawale” waliweza kutumia wananchi haohao katika nyadhifa mbalimbali ili kunyonya nchi yao. Kwasababu si kweli kwamba wakati wa ukoloni wazungu walishika nafasi zote. Walikuwa ni wakuu wa kila idara lakini wafanyaji kazi walikuwa wazalendo. Kwa ufupi wote walioshiriki katika mfumo huo walikuwa na mafunzo yaliyopelekea unyonyaji wa mali za nchi zao na kunufaisha nchi za magharibi.

Na tukitazama wagombea uhuru ambao baada ya kuona athari za unyonyaji walitamani uhuru ili waweze kufaidi matunda ya nchi zao badala ya kunufaisha wakoloni. Uhuru ulipopatikana na wakoloni kuondoka ndoto za wazalendo kufaidi matunda ya uhuru ndipo zilipogeuka kuwa majinamizi. Sababu kubwa ya matokeo ya kudidimia kwa hali za maisha ya wananchi baada ya uhuru ni kwamba viongozi waliopewa nafasi za kuongoza nchi walipoteza dira. Badala ya kufaidisha wananchi wao wakageuka kuwa ni vyombo vya wakoloni kuendelea kunyonya nchi zao. Wachache ambao hawakutaka kuwa chini ya wakoloni baada ya uhuru wakajikuta wako na hali ngumu kiasi cha kushindwa kuleta mabadiliko yoyote yenye manufaa kwa wananchi wao.

Viongozi wengi wakageuka kuwa madikteta na kukandamiza wananchi wao. Kutotumia wasomi waliokuwepo kuendeleza viwanda vilivyoachwa ilikuwa ni moja wapo ya sababu kubwa iliyopelekea kuzorota kwa maendeleo kwenye nchi nyingi za afrika ikiwemo Tanzania. Viwanda vilivyoachwa na wakoloni vikafa kutokana na kukosekana kwa ufundi na elimu ya uendeshaji viwanda hivyo.

Mpaka sasa miaka arobaini na kitu baada ya uhuru, tunatumia mifumo ileile iliyoachwa na wakoloni katika elimu, ulinzi, afya na hata usafiri. Mpaka leo mzalendo hayuko huru kutokana na sheria tunazotumia ni zilezile za mkoloni. Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wamegeuka kuwa ni wawakilishi wa serikali. Si kosa lao bali ni mfumo wanaotumia, kama wakati wa ukoloni kazi yao ni kuhadaa wananchi huku nchi ikinyonywa bila huruma na wananchi wakiendelea kuteseka bila msaada.

Mafunzo ya askari ni yale yale ya wakoloni, ukimuona polisi kimbia badala ya polisi kuwa ni wafanyakazi wa jamii katika nchi huru wamekuwa ni wafanyakazi wa serikali. Badala ya mahakama kusimamia haki za wananchi zimekuwa ni kikwazo katika kutafuta haki. Mfumo wa ukiritimba umepelekea nchi kugubikwa na wingu la rushwa ambalo athari yake ni kama saratani kwenye mwili.

Badala ya elimu kumpa mwananchi uwezo wa kuweza kutambua mazingira yake na kuyatumia ipasavyo kujiendeleza na kuinua hali ya maisha na nchi kwa ujumla, kwasasa haina athari yoyote chanya kwasababu kama ni umasikini kila kukicha hali ya wananchi wakawaida inazidi kuwa mbaya. Miaka mingi baada ya uhuru nchi nyingi za afrika zimebaki kutegemea wahisani kufanikisha bajeti ambazo hazina faida yoyote kwa wananchi wakawaida. Bajeti hizo zaidi ni kwa ajili kunufaisha walio madarakani na pia hao wahisani. Mpaka hapo viongozi wetu watakapoamua kutekeleza uhuru wa kweli katika kila nyanja wananchi tutabaki tunadidimia na hali mbaya ya umasikini.

Mdau-Mwanaharakati

Friday, 5 June 2009

Bongo hakuna wasomi



Bongo hakuna wasomi kama tafsiri yangu ya usomi ni mtu mwenye kuona tatizo akalitatua kwa kutumia elimu iliyojaribiwa (tried and tested). Msinishambulie kwasababu kama kungekuwa na wasomi tusingekuwa na shida ya maji wakati maji kila siku yanatiririka kwenye mito kuelekea baharini bila ya kupingwa.


Kungekuwa na wasomi wangejenga mazuio ya maji yasiende baharini ili yatumike kwa shughuli mbalimbali. na tusingepanga foleni zenye urefu wa maili kusubiri zamu ya kukinga dumu ili upate maji ya kunywa.


kama kungekuwa na wasomi barabara zetu zingetosha na foleni ya magari isingetungiwa nyimbo. na watu wasingetoa wazo la kugawa barabara moja njia tatu. mipango miji ingekuwa wazi na mamlaka husika wasingekuwa wakipata gharama za kuvunja nyumba za masikini na masikini kupata machungu zaidi maana kubomoa ni siku moja lakini kujenga ni kazi ya miaka.


kungekuwa na wasomi elimu ingekuwa ya manufaa na maisha ya wananchi yangeinuka na kupanda kiwango kila mwaka.


kungekuwa na wasomi huduma za afya zingetolewa bila rushwa na pia zingekuwa za uhakika wagonjwa wa miguu wasingepasuliwa vichwa na wagonjwa wa vichwa wasingepasuliwa miguu. ingekuwa ukifika hospitali una mategemeo ya kupona na si kumalizwa kabisa. wagonjwa wasingelazwa sakafuni, wagonjwa watatu wasingelazwa kitanda kimoja. na wodi za wagonjwa zingekuwa safi kuepusha maambukizi ya magonjwa.


kungekuwa na wasomi viwanja vya wazi visingemilikishwa kwa watu na badala yake kungekuwa na bustani na viwanja vya michezo mbalimbali. nyumba zingejengwa kiholela na kutengeza mijiovyo (slums) badala ya mipango miji safi.


kungekuwa na wasomi nisingeandika mada hii.....

Saturday, 20 December 2008

wacha tu tule pozi


Ni kawaida kwa mtu yeyote baada ya kazi ngumu au shughuli yeyote ni lazima apate angalau muda wa nusu saa au dakika 15 apumzike hii yote ni kwa ajili ya kuweka mambo sawa na kuipumzisha akili baada ya ya kufikiria kwa muda mrefu .huku matumbo yetu yakiwa yana joto kwa kusubiri matokeo ya form 4 ambayo kwa hakika siwezi kusema ni kwa nini hasa kwa nchi yetu kama hii ya tanzania mitihani inakuwa na matatizo kama yanayoendelea kujitokeza miaka hii ya karibuni.Naamini suala hili ni wazi kuwa wizara husika ndiyo ishugulikie makini

Wednesday, 28 May 2008

Vitambulisho Vya nini?


Vitambulisho vya nini katika nchi ambayo hata umeme wa uhakika bado ni changamoto. Mabilioni ya pesa ambayo yangeweza kuhakikisha shule zina vitabu vya kutosha, hospitali zina dawa za kutosha, barabara zinapitika japo kwa msimu wa kiangazi, watu wanaajira japo za kuhakikisha mlo mmoja kwa siku. Vitambulisho vya nini wakati passport zinatosha kumtambulisha mwananchi, vitambulisho vya nini wakati gharama za utengezaji ni kubwa kuliko kipato cha mlengwa. gharama za utunzaji wa kitambulisho hicho ni nani atakayelipa maana kama ni kitambulisho kilichotengezwa kwa kutumia plastiki kina "finite life time", nani atakayelipa "replacement" ya kitambulisho hicho. na kama kitakuwa na "Chip", je vifaa vya kusomea habari zilizopo kwenye hiyo chip vitawekwa kila ofisi iwe ya serikali na binafsi. kwa ufahamu wangu inabidi uwe na central database system ambayo itashughulikia uhifadhi wa habari za mwenye kitambulisho, mambo yanayohitaji kuwa na ma "computer servers " kubwa na pia watu wa kuendesha computer hizo na pia umeme wa uhakika na sio wa mgao si kwenye hizo computer farms bali na hizo "service points". faida za mradi huu kwa hakika zinashindwa na hasara zitakazopatikana, na si baada ya muda mrefu mradi utakufa na mabilioni yaliyotumika yatakuwa ni kama maji yaliyomwagika mchangani. hizo pesa zingetumika katika kutatua matatizo yanayomgusa mtanzania kila siku kama vile upatikanaji wa maji safi "on demand", upatikanaji wa huduma bora za afya na gharama nafuu, upatikanaji wa elimu bora yenye kwenda na wakati kwa gharama nafuu... VIONGOZI WETU WALIOPEWA MADARAKA YA KUFANYA MAAMUZI KWA MANUFAA YA TAIFA WANAFANYA MAAMUZI KWA MANUFAA YA KWAO WENYEWE..TATIZO TULILONALO WAAFRIKA SIO UMASIKINI WA PESA, BALI UMASIKINI WA FIKRA NA ELIMU NDIO UNAOTUANGAMIZA ZAIDI...

Monday, 11 February 2008

Tanzania Bila Rushwa Na Ufisadi Inawezekana


Kila kona ya mitaa ya Bongo utakuta bango kubwa lenye ujumbe kama linavyoonekana kwenye picha, hapo juu...ningependa kuona mabango kama hayo yenye ujumbe usemao TANZANIA BILA RUSHWA NA UFISADI INAWEZEKANA TUWEKE MIFUMO WAZI....Nimefurahi kuona wabunge wote wameungana kupigania maslahi ya wananchi badala ya kutetea maslahi ya wachache wenye tamaa zisizokuwa na mipaka katika kujikusanyia mali kwa njia zisizo halali hivyo kuhatarisha uchumi wa nchi. Muda wa kulindana umekwisha, muda wa UKADA umekwisha sasa tushirikiane wote waliopewa madaraka na wasiokuwa na madaraka, tubadili misimamo yetu kwa maslahi ya nchi kwa ujumla. ningependa kuona Rais katika baraza jipya kuna waziri japo mmoja toka katika kambi ya "UPINZANI" ili kutoa ishara kuwa michango yao katika bunge inalenga kutetea maslahi ya taifa na wananchi wake kwa ujumla, tuondokane na siasa za chuki za kuona hata kama mpinzani akileta hoja yenye kutetea wananchi basi chama tawala lazima kipinge kwa nguvu zote. Huu ni muda wa kushirikiana wote tulete maendeleo ya nchi kwa haraka..Tumechoka kuitwa nchi masikini wakati UTAJIRI wetu unachukulia hivi hivi tungali macho tena wengine tunasaidia kubeba kupeleka nje ya nchi huku wananchi wanaishi kwenye mabanda ya mabati mabovu yaliyofunikwa kwa maplastiki...

hakuna ajira vijana wamebaki kuwa wakabaji na majambazi...madada nao wamekuwa wakijiuza kwenye kwenye kona za jiji...