Wednesday 2 September 2009

UMASIKINI AFRIKA-NI WAPI NDOTO ZA MATUNDA YA UHURU ZILIPOGEUKA JINAMIZI

Ukitazama historia ya nchi nyingi za afrika wakati wa kupigania uhuru toka kwa wakoloni utagundua kuwa japo ilikuwa lazima mwafrika awe huru lakini wapigania uhuru hawakuwa na mipango madhubuti ya kuendesha nchi zao baada ya kupata uhuru huo. Miaka ya sitini ndio ilikuwa kipindi cha mabadiliko sehemu nyingi duniani zikiwemo nchi za magharibi. Kipindi hicho mabadiliko ya mtazamo wa jamii kuhusu maisha hasa katika nchi za magharibi ulikuwa chachu kwa nchi zilizokuwa chini ya wakoloni kujikomboa.

Kutokana na ukweli kwamba wazungu wasingeweza kuendelea kushikilia makoloni yao kutokana na harakati za kipindi hicho hawakuwa na budi kutoa uhuru kwa nchi walizokuwa wakizishikilia kama makoloni. Ulazima wa kutoa uhuru na ulazima wa kuendelea kunyonya makoloni hayo ulisababisha maamuzi magumu kufanyika. Na hapo ndipo mwanya wa kuchukua baadhi ya hao wagombea uhuru na kuwasomesha katika vyuo vikuu vyao ili kuwaandaa kuchukua hatamu za nchi zao. Ni ukweli usiopingika kuwa wagombea uhuru hao walikuwa na ndoto njema juu ya mafanikio yatakayopatikana baada ya kupata uhuru. Wananchi waliokuwa na matumaini ya kupata maisha bora zaidi ya waliyokuwa nayo kabla ya uhuru walitoa nguvu zao zote kufanikisha azma ya kuwa huru.

Tukitazama jinsi ya wakoloni walivyoweza kutawala tunaona jinsi walivyoweka mipango bora iliyosukwa rasmi katika kufanikisha unyonyaji wa mali toka kwenye makoloni hayo. Ukianzia ulinzi, ambapo ni jambo la muhimu sana katika unyonyaji, wakoloni waliweza kuweka majeshi ya polisi yaliyofunzwa mafunzo maalum ya kutia woga na hofu kwa wananchi ili wasiweze kuvuruga amani na kusababisha shughuli za unyonyaji kusimama. Pia waliweza kujenga njia za usafiri zilizowezesha kusafirisha mali kwa urahisi. Waliweka mfumo mzima ambao kwa kutumia njia ya “kuwagawa ili uwatawale” waliweza kutumia wananchi haohao katika nyadhifa mbalimbali ili kunyonya nchi yao. Kwasababu si kweli kwamba wakati wa ukoloni wazungu walishika nafasi zote. Walikuwa ni wakuu wa kila idara lakini wafanyaji kazi walikuwa wazalendo. Kwa ufupi wote walioshiriki katika mfumo huo walikuwa na mafunzo yaliyopelekea unyonyaji wa mali za nchi zao na kunufaisha nchi za magharibi.

Na tukitazama wagombea uhuru ambao baada ya kuona athari za unyonyaji walitamani uhuru ili waweze kufaidi matunda ya nchi zao badala ya kunufaisha wakoloni. Uhuru ulipopatikana na wakoloni kuondoka ndoto za wazalendo kufaidi matunda ya uhuru ndipo zilipogeuka kuwa majinamizi. Sababu kubwa ya matokeo ya kudidimia kwa hali za maisha ya wananchi baada ya uhuru ni kwamba viongozi waliopewa nafasi za kuongoza nchi walipoteza dira. Badala ya kufaidisha wananchi wao wakageuka kuwa ni vyombo vya wakoloni kuendelea kunyonya nchi zao. Wachache ambao hawakutaka kuwa chini ya wakoloni baada ya uhuru wakajikuta wako na hali ngumu kiasi cha kushindwa kuleta mabadiliko yoyote yenye manufaa kwa wananchi wao.

Viongozi wengi wakageuka kuwa madikteta na kukandamiza wananchi wao. Kutotumia wasomi waliokuwepo kuendeleza viwanda vilivyoachwa ilikuwa ni moja wapo ya sababu kubwa iliyopelekea kuzorota kwa maendeleo kwenye nchi nyingi za afrika ikiwemo Tanzania. Viwanda vilivyoachwa na wakoloni vikafa kutokana na kukosekana kwa ufundi na elimu ya uendeshaji viwanda hivyo.

Mpaka sasa miaka arobaini na kitu baada ya uhuru, tunatumia mifumo ileile iliyoachwa na wakoloni katika elimu, ulinzi, afya na hata usafiri. Mpaka leo mzalendo hayuko huru kutokana na sheria tunazotumia ni zilezile za mkoloni. Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi wamegeuka kuwa ni wawakilishi wa serikali. Si kosa lao bali ni mfumo wanaotumia, kama wakati wa ukoloni kazi yao ni kuhadaa wananchi huku nchi ikinyonywa bila huruma na wananchi wakiendelea kuteseka bila msaada.

Mafunzo ya askari ni yale yale ya wakoloni, ukimuona polisi kimbia badala ya polisi kuwa ni wafanyakazi wa jamii katika nchi huru wamekuwa ni wafanyakazi wa serikali. Badala ya mahakama kusimamia haki za wananchi zimekuwa ni kikwazo katika kutafuta haki. Mfumo wa ukiritimba umepelekea nchi kugubikwa na wingu la rushwa ambalo athari yake ni kama saratani kwenye mwili.

Badala ya elimu kumpa mwananchi uwezo wa kuweza kutambua mazingira yake na kuyatumia ipasavyo kujiendeleza na kuinua hali ya maisha na nchi kwa ujumla, kwasasa haina athari yoyote chanya kwasababu kama ni umasikini kila kukicha hali ya wananchi wakawaida inazidi kuwa mbaya. Miaka mingi baada ya uhuru nchi nyingi za afrika zimebaki kutegemea wahisani kufanikisha bajeti ambazo hazina faida yoyote kwa wananchi wakawaida. Bajeti hizo zaidi ni kwa ajili kunufaisha walio madarakani na pia hao wahisani. Mpaka hapo viongozi wetu watakapoamua kutekeleza uhuru wa kweli katika kila nyanja wananchi tutabaki tunadidimia na hali mbaya ya umasikini.

Mdau-Mwanaharakati

No comments: