Tuesday, 16 October 2007

Maendeleo Na Elimu toka Mwaka 47

Elimu ya tanzania katika ngazi ya shule ya msingi mpaka chuo kikuu inatia uchungu sana kutokana na ukweli kuwa haiendi na wakati. Wakati elimu ndio ingekuwa chachu ya kujua umuhimu wa kwenda na wakati, elimu yetu imebaki kama tulivyoachiwa na wakoloni.

Nashangaa hata huko chuo kikuu bado wanaendelea kutumia vitabu vilivyopitwa na wakati wakati teknolojia ya habari(IT Technology) imefungua milango ya elimu duniani ambapo wasomi wanaweza kubadilishana mawazo bila kujali kama wapo katika kona gani ya dunia. Elimu ya Uchunguzi (Research) katika mada mbalimbali ni muhimu kwa nchi yenye kujua umuhimu wa elimu ili kutatua matatizo yanayowakabili bila kusubiri kuiga kutoka kwa wageni .

Jawabu la tatizo fulani katika jamii fulani haliwezi kuwa jawabu la tatizo hilohilo katika jamii nyengine na hii inatokana na mambo mengi yanachangia kuwa na sababu ya kutafuta jawabo la tatizo hilo kwa kufanya uchunguzi kwenye jamii husika. Ni kosa ambalo kama msomi naliona likirudiwa mara kwa mara katika nchi za kiafrika ambapo badala ya kutilia mkazo kwenye kuboresha kiwango cha elimu watoayo kwa wananchi wao wamebaki ku-copy na ku-paste toka kwa nchi nyengine wakidhani itakuwa jawabu la matatizo yanayowakabili na hii inafanya nchi kuzunguka duara na kurudia kwenye tatizo lile lile badala ya kwenda mbele.

Nchi zilizoendelea zimeweka mkazo maalum kwenye vyuo vitoavyo elimu ya juu kuhakikisha kwamba research mbalimbali zinafanyika na kusaidia jamii kujikwamua katika matatizo mbalimbali yanayoikabili. Bila dhamira na Utekelezaji wa vitendo katika kuhakikisha elimu itolewayo ina manufaa kwa jamii husika Afrika hatutaweza kujikwamua katika dimbwi hili la Umasikini.

No comments: