Wednesday 2 January 2008

DemoCrazy Vs DemoCracy

Hivi lini Waafrika tutaamka na kuanza kuishi kama wanadamu walioendelea badala ya kubaki na fikra za kinyama, hadaa, uonevu, mauaji ya halaiki kwa tamaa za kubaki kwenye madaraka ama kutwaa madaraka bila ya idhini ya wananchi.

Waafrika baada ya kupigania uhuru toka kwa wakoloni, mababa zetu waliunda serikali chini ya chama kimoja na kuwaunganisha wananchi wote bila kujali dini, kabila na rangi zao. Japo maendeleo hayakuja kama wengi walivyotarajia na hii inatokana na ukweli kwamba nchi nyingi zilipata uhuru bila kuwa na wasomi wa kutosha wa kuendeleza rasilimali zilizoachwa na wakoloni, kwa hiyo nchi nyingi zikatumbukia kwenye dimbwi la umasikini.

Viongozi walioko madarakani wakawa wanyonyaji kwa kujinufaisha binafsi bila kujali hali halisi za wananchi wao, na hapo migogoro ikazuka na pia ukabila ukaibuka na hatimaye vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya nchi. Ukitazama historia, tumekuwa watumwa, tumenyonywa, na tuaendelea kunyonywa kwasababu hatuna umoja kila mtu kivyake.

Miaka ya Tisini nchi za magharibi zikalazimisha Afrika kuwa na vyama vingi kwa jina la DEMOKRASIA, kwa mtazamo wao ilikuwa ni kutugawanya ili waweze kutunyonya zaidi kwa kufunga mikataba na yeyote atakayekuwa madarakani na kama hao walioko kwenye madaraka hawataki basi wapinzani wao watapewa misaada ili waingie kwenye madaraka hivyo kuhakikishwa kwa upande wa mataifa ya Magharibi ni 'win win situation' , kwa mtazamo wa viongozi walikuwa madarakani wakapata nafasi pia kugawanya wananchi, wenye madaraka na WAPINZANI.

Kwa mtazamo wa viongozi wa kiafrika tukapata DEMOCRAZY, wananchi wakagawika pande mbili kama mashabiki wa timu za mpira wakifuata viongozi wao bila kujali kama hao viongozi wanajali maslahi yao binafsi ama maslahi ya nchi kwa ujumla. viongozi wetu wametuingiza katika hali mbaya za kuvunjika kwa amani kwa maslahi yao binafsi nasi wananchi tunaburuzwa na kuumia, kupoteza maisha wakati viongozi wetu wakiwa katika mahekalu yao yalijaa ulinzi wakibweka amri zenye kutumaliza.

Lini tutajifunza kuwa yaliyotokea Rwanda, na Burundi yanaweza kujirudia kama mambo yalivyo Kenya hivi sasa. Wachache wenye uchu na tamaa za kubaki katika viti vya enzi kwa gharama za maisha ya wananchi wasio na hatia wataendelea kutuchimbia makaburi kabla ya muda mpaka lini. AFRIKA HAKUNA DEMOKRASIA ILA KUNA DEMOCRAZY na wanaoumia na wananchi wa kawaida.

part1....to be continued

No comments: