Monday 20 August 2007

Tutazame Utoaji wa huduma za Afya...

Jua limeshachomoza na harakati za kutafuta mlo wa leo zilishaanza mapema wavuvi washaelekea baharini na nyavu zao, wakulima nao njiani kuelekea mashambani. Wanafunzi vituoni kusukumana na makonda wa daladala kuelekea shuleni.

Katika mambo muhimu ambayo yanamhusu mwanadamu popote alipo ni huduma za afya hasa ukizingatia huku uswahilini ikipita miezi mitatu hujaugua Malaria ni bahati kubwa maana Mbu hushambulia hata ukiweka neti ya dawa mbu nao siku hizi huimba "ALUTA KONTINUUUUAaaa", na ukiamka utakuta wamejaza kibao ndani ya neti matumbo yao mekundu yamejaa mlo wa damu yako.

Uswahilini hakuna bima ya afya, DINGI anasema nikakate bima ya afya wakati BIMA ya Mlo wa Mchana sina. ndio hivyo ukiumwa huna budi kwenda kumuona daktari baada ya maji ya Mwarobaini kushindwa kukutetea dhidi ya mashambulizi ya vimelea ya Malaria. Hapo ndipo kasheshe linapoanza maana kabla daktari hajakutupia jicho inabidi ulipe ili macho yake yafunguke. na hapo baada ya kulipa hicho kiingilio cha kuonekana na daktari ndipo utasikia "HAYO NI MALARIA TU!!", anakucheki kwenye magoti huku akikuuliza "je UNASIKIA UCHOVU KWENYE MAUNGO?" .Na jibu ni lile lile la ndio na ukibadilisha hakuna mabadiliko katika vipimo nenda kapime damu pale kidirishani, ukienda hapo kidirishani kuna " MICROSCOPE" Imechoka na hata ya pale shuleni kwetu ina nafuu, jamaa akishakutoboa kwenye kidole anaweka chini ya kioo cha darubini yake huku akifinya jicho kuchungulia kilichomo, baada ya sekunde kadhaa utakuta keshaorodhesha mpaka idadi ya vimelea alivyokuta ndani, "Haya Tayari Nenda Kamuone Daktari".
Ukifika huko kwa daktari, hicho cheti chako ataandika kwa mwandiko ambao ni yeye tu na manesi ndio wanajua kusoma sasa nauliza kwani "KUNA SIRI GANI KWENYE CHETI CHA HOSPITALI MPAKA MUANDIKE KAMA CODED MESSAGE", miandiko kama kapita kuku, kila mwandiko ukizidi kuwa mbaya ndio daktari anajisifia kuwa ndio daktari bingwa, na dozi ni ile ile SINDANO, NA MIDONGE YA FANCIDA. wakati mwengine namwambia dingi ni bora tutumie cheti cha miezi mitatu ilopita maana tiba na ugonjwa ni uleule, badala ya kwenda kulipa kiingilio halafu juu yake ulipie matibabu. Ndio maana wananchi wengi hukimbilia kwa Waganga wa JADI kwa kuwa hakuna kiingilio japo hao WAGANGA WA JADI wakiumwa hukimbilia hospitali..
Na hapo umeumwa malaria tu ukienda kulazwa hospitali za wilaya utaona jinsi wagonjwa wanavyo-share vitanda bila kujali ugonjwa uliowapeleka hospitali. Manesi wanajitahidi kutoa huduma lakini hakuna motisha wa kutosha wakuwafanya wapende kazi yao, Mie nadhani hufanya kazi ile kwa mapenzi na huruma waliyonayo ndani roho zao na si vinginevyo kwa maana mishahara yao haikidhi mahitaji yao.
Madaktari wao afadhali wanafanya kazi mbili kwa wakati mmoja, Kaajiriwa na hospitali ya serikali lakini muda wote yuko kwenye hospitali yake uchochoroni, ukiulizia utaambia daktari hayupo lakini ukionyesha noti utapewa maelekezo aliko huko kichochoroni.. ATAFANYAJE WAKATI AKILILIA ONGEZEKO LA MSHAHARA serikali inamfukuza kazi, si bora awe anafanya Overtime pembeni UKIZINGATIA ana familia na extended-familia na marafiki pia wanamtegemea. Na hayo ndio mambo SIKU ZOTE OMBA AFYA NJEMA ndio jambo muhimu..

No comments: