Friday, 27 May 2011

Barua Yangu Kwa Raisi

Mheshimiwa Baba Raisi wa nchi yangu,

Ni mimi mwanao Shida na ndugu yangu Tabu, tumeona leo tuandike barua kwako ili uweze kukumbuka hali zetu. Sisi tuwazima japo wiki iliyopita Malaria na Kipindupindu kilitaka kutuhamisha duniani. Natumai nawe umzima wa afya na uko katika pirika pirika za kutuletea unafuu wa maisha.


Juzi nilimuona Mjomba WAZIRI akipita na gari lake lenye vioo vyeusi njiani wakati natoka kumtazama bibi majuto. Pengine kutokana na weusi wa vioo na jua lilikuwa likituchoma hakuweza kutuona na hivyo tulichoambulia ni vumbi.

Nakukumbusha kuwa huku kwetu jua bado linawaka kwenye mifuko ya suruali ya kila ninayepishana nae njiani. Kwa hiyo naomba utuangazie macho nasi tupate kuona maana njaa inazidi kutukosesha amani. Vijana wamejiajiri kukosha magari ya wapitao lakini wengine wanaouza mahindi na maji purukushani na Mgambo haziishi.

Sina imani tena kila nikimuona polisi nakimbia badala ya kumsogelea ili anilinde kwasababu majuzi Tabu aliwekewa kipande cha bangi mfukoni na kuambiwa ni mzururaji pia. Mimi nimechoka kuomba omba njiani kila nikijiajiri naona watumishi wako wananijengea vizingiti nishindwe kupita. Kwa hiyo nakuomba utupunguzie matatizo yaliyo ndani ya uwezo wako na natumai unayajua maana yalikuwa katika zile ahadi ulizotoa wakati wa uchaguzi..


Ndimi Shida na ndugu yangu Tabu

No comments: