Tuesday, 7 June 2011

Jawabu la kauli ya Madaraka kuhusu Ujenzi wa barabara katika Mbuga ya Serengeti.





Baada ya kusoma kauli mada iliyotolewa na Ndugu Madaraka Nyerere kuhusu ujenzi wa barabara katika mbuga ya kuhifadhia wanyama ya Serengeti nimeona na mie niseme jambo.
Kwanza kabisa nianze kwa kusema nimesikitishwa na mawazo ya Ndugu Madaraka kuhusu katika kufananisha athari ya ujenzi wa barabara na mapito ya wanyama hao katika maeneo yenye wanyama wakali kama simba na mito iliyojaa mamba. Amesahau kuwa kuwepo kwa wanyama wanaokula wanyama wenzao (Predators) ni msawazo maalum katika mizani ya maisha ya wanyama hao. Wenye kula majani wanategemea wanyama wanaowinda katika kuhakikisha kuwa idadi yao inahimili mazingira waliyopo. Na pia Simba na wanyama wawindaji huchunguza kundi kabla ya kuwinda wakiona mwenye matatizo (weak) ndio wanamuwinda hivyo kuacha wenye afya njema wakiendelea.
Athari ya barabara katika mbuga sio tu kwamba itabomoa natural order ya wanyama hao bali itabadili mazingira, je umefikiria suala la uchafuzi wa mazingira utakaotokana na gesi chafu za magari (air pollution) na kemikali zitakazomwagika kama mafuta ya magari, sauti za magari(sound pollution), uchafu utakaotupwa ovyo na wapiti njia, idadi ya wanyama watakakufa kwa kugongwa na magari, njia rahisi kwa majangili kuuwa wanyama hao, idadi ya askari pori watakaohitajika kulinda wezi wa nyara, uharibifu wa mioto asilia na kujenga mipaka isiyo asilia. Hayo ni kwa upande wetu na jinsi gani wanyama watakavyopokea kuwepo kwa barabara na mambo yatakayoletwa na hiyo barabara.
Tumekuwa masikini katika upande wa kuelewa mazingira yetu kiasi leo ni wageni wenye utaalamu katika kuelezea maisha na tabia za wanyama wanaoishi kwenye mbuga zetu kiasi sisi tumebaki wabeba vifaa ya kupigia picha na wapelekaji wa watu porini.
Tumeshindwa kufahamu tabia za wanyama na faida zao kiasi tunawaona kama kikwazo kwetu badala ya kuwa ni tija yenye thamani kuu. Leo hii tukimuona mbwa tunaokota jiwe kumpiga bila sababu wala fikra wakati mbwa huyo anaweza kutumika kutambua magonjwa kama Cancer katika mwili wa binadamu, ama kutambua kuwepo kwa dawa za kulevya ama silaha.
Leo hii wanasayansi wanamsoma Inzi kutambua uwezo wake wa ajabu wa kuweza kuruka na kutua katika dari ili waweze kuigiza katika mifumo ya kuendesha ndege lakini kwangu wewe na mimi tunamuona si kitu. Leo hii wanasayansi wanamsoma mjusi kutambua uwezo wake wa kutembea kwenye kuta na glasi ili waweze kutengeza gundi lakini kwangu mie na wewe tunaona bora tumpige fagio afe. Leo hii wataalamu wanatambua kwanini Simba dume halei watoto wa kambo kwangu mimi na wewe hii ni hadithi.
Leo hii tunachoona ni barabara tu bila kufikiri kuwa barabara si lami tu ilotandazwa bali ni mfumo mzima wenye taathira kuu kila inapopita. Kuhifadhi mazingira ni jukumu la taifa zima na kuwepo kwa mbuga iwe ni chachu ya kutambua umuhimu wake kuwepo pale.
Leo hii wanyama kama Simba wameingizwa kwenye Listi ya wanyama watakaopotea baada ya miaka michache inayokuja kutokana na shughuli za binaadamu kuhamia katika mazingira yao hivyo kuzuia mihamo yao kutoka katika familia walizozaliwa kwenda kuhamia kwenye familia nyengine ili kuepusha kuzaliana wenyewe kwa wenyewe na hiyo kusababisha madhara ya uzaofinyu (Inbreeding). Kwa hili hata sisi binadamu tunaweza kujifunza lakini kwasababu ya umasikini wa fikra hatulioni hili.
Suala la kusema mahitaji ya wanyama yamewekwa mbele zaidi ya binadamu kwanza tukumbuke kuwa binadamu ni mnyama pia. Na katika mfumo mzima wa maisha wanyama wote wana mchango maalumu katika kuwepo kwao. Kutokana na ubinafsi wa binadamu na kujifanya kuwa na akili nyingi tumeharibu sehemu nyingi za mfumo huu kiasi taathira zake zimekuwa zikituangamiza sisi wenyewe.
Tanzania tumebarikiwa kuwa na utajiri asilia ambao ni bora kuliko faida ya hiyo barabara. Tunachotakiwa ni kufahamu utajiri huo na kuuthamanisha ili tuweze kupata tija. Wenzetu wa nje sio kwamba wanatukwaza bali kutokana na ukosefu wa elimu na kutoona mbali tulionao wanatuonea huruma tukija kupoteza utajiri huu tutakwenda kwa nani.
Wazungu waliwaua wanyama wenye kuwinda na kuwindwa kwenye nchi zao baada ya miaka mia ndio wakaona taathira waliyofanya na sasa wanatumia mabilioni ya pesa kurudisha wanyama hao ili wabalance ile natural order iliokuwepo. Leo hii kwenda kutazama ndege kipanga inabidi uombe leseni na hupati leseni hiyo bure ni lazima watizame historia yako, sie kwetu bure tunawaona wasumbufu wanaotuibia kuku. Dar es salaam kulikuwa na ndege kila aina miaka ya tisini leo hii waliobaki ni kunguru je unaijua sababu?
Watanzania tuache maneno ya kisiasa penye kuhitajika utaalamu..inaonyesha tuko tayari kuuza shamba kwa mlo wa leo tu..
Mungu Ibariki Tanzania na Tupe ufunuo katika fikra zetu.
Mdau Mwanafunzi.

No comments: