Friday, 10 June 2011

UWELEWA WA UTAJIRI WA MAZINGIRA NA MAENDELEO YA MWANADAMU

Kwanza kabisa nianze kwa kusema kuwa Mwenyezi Mungu ametubariki kwa utajiri wa maliasili uliotukuka katika nchi yetu ya Tanzania. Tukianzia kwenye Bahari na mpaka Maziwa. Ni nchi pekee katika bara la afrika kuzungukwa na maziwa makuu matatu. Yenye uoto wa asili na ndipo panaposadikiwa kuwa mpaka sasa inasadikika kuwa binaadamu wa kwanza alitoka hapa kutokana na rekodi za fuvu lililovumbuliwa kule Olduvai Gorge. Tuna mbuga nyingi lakini katika mbuga hizo Serengeti ndio kinara wa mbuga zote duniani kwa kuwa na mkusanyiko mkubwa wa wanyama katika eneo moja.
Tokea enzi za zama uhusiano wa binaadamu na mazingira yake umekuwa ndio chachu ya maendeleo yake. Kutokana na uwezo wetu wa kufikiri tumeweza kuyafanya mazingira yetu kuwa nguzo kuu ya utegemezi na ni mhimili wa kuwepo kwetu. Mara zote tumeweza kuchukua kila kinachotoka kwenye mazingira yetu kwa faida yetu bila kujali athari kwasababu tunaona dunia ni kubwa hivyo athari zetu ni kidogo. Wengi wetu tunaamini kuwa dunia ina malighafi isiyokwisha (infinite resource) lakini ukweli ni kwamba kuna idadi maalum ya malighafi iliyopo duniani hivyo tunapotumia ikiisha tufahamu kuwa vizazi vinavyokuja vitasumbuka kwa kurithi deni la malighafi ambalo hawataweza kulipa na hivyo kwa wenye kujua hesabu kuna kitu kinaitwa mapato yenye kupungua (diminishing returns).
Hii imetokea kwenye miji mingi ya kizamani ambapo wakaazi walitumia malighafi zao kwa fujo na baada ya kuisha na wao maisha yao yakawa hatarini hivyo wenye uwezo walihama kwenda sehemu nyengine na wasiojiweza wakaishia kupoteza maisha. Leo hii nchi zimewekwa mipaka hivyo kuhama si suala la kufikirika. Ndio maana wamarekani wanafikiria kuhamia kwenye sayari nyengine ili wapate malighafi toka huko. Na kugombea malighafi ndio chanzo cha vita vyote kuanzia wanafamilia mpaka nchi na nchi nyengine.
Sasa tuangalie katika nchi yetu na malighafi tulizonazo na nini tunafanya. Tumewapa wawekezaji panga wajikatie mapande wanayotaka ili mradi watupe asilimia chache za mapato na kuwapa msamaha wa kodi. Upande wa madini tunawaachia wakivuna dhahabu tani kwa tani bila kufahamu dhahabu huisha na zikiisha na wawekezaji nao watahama kurejea kwao na sie tutabaki na simulizi za mashimo matupu na taathira za mazingira tutakazobaki nazo miaka mingi inayokuja kutokana na kemikali za sumu zinazotumika kuchimbia dhahabu hizo. Vizazi vijavyo watapata simulizi tu jinsi tulivyokuwa matajiri bila kuona faida ya utajiri huo (Lodi Lofa).
Wenzetu wanafikiria watakuwa wapi baada ya miaka mia tatu ijayo na kufanya kila aina ya hesabu kujua hatma yao kutokana na mahitaji ya jamii na malighafi zilizopo, sie tunajali ya leo tu tukishapewa ten percent tunauza urithi ili mradi tupate kuendesha Hummer na Lexus. Tunaangalia idadi ya watanzania kama ni tatizo badala ya kuwa ndio jawabu la matatizo mengi tunayongojea wageni watusaidie. Ukweli ni kwamba hakuna msaada wa bure siku zote ni “nipe nikupe”, hii ndio inayovutia nchi nyengine kuwekeza kwenye nchi ngeni ili waweze kujaliza mapungufu yao. Na kama huna mipango maalum ya kudhibiti matumizi ya malighafi yako ndio unakuwa kivutio kikuu.
Nchi nyingi za Afrika zimekuwa ndio waongozaji wa kutoa malighafi na pia kugeuzwa soko la bidhaa zinazotokana na malighafi hizo. Kiasi ni biashara yenye kulipa sana kwasababu nanunua malighafi kwa shilingi moja natengeza kitu nakuuzia shilingi kumi.. halafu unashangaa kwanini deni la taifa linazidi kila dakika inayopita.
Suluhisho ni kuweka kipaumbele elimu zote na kuweka umuhimu zaidi katika ufundi uhandisi(engineering) ili tutengeneze viwanda ili sisi wenyewe tutumie malighafi zetu na pia kupata ajira za uhakika tutengeneze bidhaa tuuzie wananchi wetu hivyo kuinua hali ya maisha yetu tujiendeleze wenyewe kisayansi na kiteknolojia badala ya kutegemea bidhaa zilizokwisha tengenezwa (finished products). Najua wengi mtapinga kutokana na nadharia ya kupata pesa chap chap lakini pesa unazopata bila mpango hupotea pia bila mpango. Na wenye fikra walisema kama hupangi mipango ya kufaulu basi mipango ya kufeli hujipanga yenyewe.
Na tuanzishe mipango maalum ya kuwavutia watoto wetu katika kuelewa na kuheshimu mila na itikadi zetu na mazingira tunayoishi ikiwamo miti na wanyama waliomo kwasababu tumezaliwa katika nchi hii kwa sababu maalum. Basi na tujue jukumu letu katika hayo kwasababu wazee wetu hawakupigana kufa kupona ili tuwe huru halafu turudi tena kwenye utumwa wa kileo. Na hayo ninayosema yanawezekana kwasababu nchi kama Malaysia miaka 30 iliyopita ilikuwa maskini leo hii ni moja ya nchi tajiri kutoka na mikakati ya kujiendeleza waliyoweka. Leo hii wamekumbatia Sayansi na Teknolojia ya kweli kiasi wengi wenu mnapeleka huko watoto kusoma. Basi nasi tufumbue macho tuweze kuona...
Mungu Ibariki Tanzania, na Utupe ufunuo na Upendo kwenye fikra zetu.
Mdau Mwanafunzi.

3 comments:

Madaraka said...

Wewe ni mwanafunzi wa masomo gani?

mwanafunzi said...

Mimi ni mwanafunzi wa masomo ya sayansi, namalizia PhD katika masuala ya Quantum Physics.

Madaraka said...

Kuna tofauti kubwa kati ya kutoa hoja mbele ya hadhira, na ya kujenga hoja kati ya watu wawili.

Nitakuandikia barua pepe.