Friday 24 June 2011

MTAZAMO WANGU KUHUSU MADA YA JOHN MASHAKA NA MAJIBU YA HASSAN

Baada ya kusoma makala zote mbili za Ndugu Mashaka na Hassan, naona niweke mtazamo wangu pia katika mada hii nyeti. Kihistoria nchi za magharibi na mashariki zimekuwa katika ushindani mkubwa wa kuboresha uchumi wa nchi zao. Na katika kuboresha uchumi MALIGHAFIndio kuchocheo kikuu katika kukuza viwanda na uzalishaji bidhaa ambazo pia zinahitaji soko la kuuziwa. Katika karne iliyopita makampuni mengi yaliyokuwa katika nchi za magharibi zilihamisha uzalishaji toka nchi zao na kuanzisha viwanda katika nchi za mashariki hasa CHINA kwasababu ya urahisi wa gharama za uzalishaji (cheap labour).
Hii ilileta ufunuo mpya kwenye nchi yenye kuhubiri UKOMUNISTI na ikaleta kubadilika kwa sera za uchumi za nchi na hivyo kujikurubisha hasa kwenye mfumo wa kibepari unaoendeshwa kinyonyaji. Maendeleo ya viwanda CHINA vimesababisha mfumuko wa tofauti kati ya walionacho na wasionacho ambao hauendani na sera zao za KIKOMUNISTI. Katika nchi yenye watu bilioni zaidi ya moja, ni wachache wenye utajiri wa ajabu kama mfano aliotoa ndugu Hassan na waliobaki ni masikini hata wengine ni masikini zaidi ya WAAFRIKA.
Swali linakuja KWANINI AFRIKA?...hapa ukweli ni kwamba si WACHINA tu wenye tamaa ya kujifaidisha kutokana na malighafi zilizoko katika bara la afrika hata hawa wa MAGHARIBI (marekani na nchi za ulaya) wamekuwa wakilitumia bara la AFRIKA kama shamba la BIBI toka enzi walipotambua kuwa kuna bara la AFRIKA.
JE WAAFRIKA TUFANYEJE? Hili ni swali ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza kwasababu mpaka jirani aje kukuomba chumvi ujue ameishiwa ama ana mipango ya kutumia yako ili yake imfae baadae. Kwa bahati mbaya kwetu ama nzuri kwao tumekuwa tukiongozwa na viongozi wenye upeo wenye urefu wa kope za macho yao kwa hiyo hawa majirani zetu kupitia mazingira ya kutusaidia wameweza kutupumbaza kiasi cha kutoona UTAJIRI TULIONAO. Tuchague viongozi wenye kuona shida zetu na kuzitafutia suluhu na pia wenye UZALENDO na upendo wa kuona wote tunafaidi keki ya TAIFA na pia kujali vizazi vyetu vijavyo na kuvilinda ili viweze kurithi mirathi bora.
Na ukosefu wa ELIMU umetufanya tusiweze kuona umuhimu wa kutumia na kulinda mali zetu kwa faida yetu hivyo tunakaribisha majirani walime wavune watuuzie mazao kwa bei wanayotaka wao. Si kwamba sipendi majirani lakini kama jirani macho yake ni kuninyonya kwasababu sijapata uwezo wa kutambua umuhimu wa nyumba yangu huyo si jirani mwema. Kwa ndugu Hassani ni kweli CHINA ilijenga viwanda na pia ikajenga TAZARA lakini ujue CHINA ya mwaka 70 si CHINA ya mwaka 2011. Na Pia NCHI za magharibi ni zile zile zilizotunyonya na mpaka sasa zinaendelea kutunyonya bila kujali huku wakitupachika jina la UMASIKINI wakati utajiri wao unatokana na MALIGHAFI ZETU.
WAAFRIKA tunahitaji viongozi wenye UZALENDO wa nchi zao wenye kujua umuhimu wa wananchi wao ili kama ni kufaidi matunda ya nchi basi tufaidi sote badala ya kujigawia kijambazi mali za MATAIFA yetu kwa kisingizio cha uwekezaji wakati mikataba ya UWEKEZAJI huo yanafaidisha upande mmoja. Lazima viongozi wetu wawe na NGUVU ya kusema kuwa kama unataka kuwekeza NGUVU KAZI lazima iwe ya humu ndani hatutaki uwekezaji ambao ni uhamishaji wa watu toka CHINA ama MAGHARIBI kuja kufanya kazi ambazo wenyeji wanaweza kufanya na kama unahitaji wataaluma basi chukua wazalendo wapewe mafunzo wawe wataaluma.
LAZIMA tuamke na kujua malighafi zina idadi maalum zikiisha tutafanya nini wakati hatufaidiki nazo wakati zipo...VIONGOZI WETU MTUONEE HURUMA NA KUTAMBUA HALI ZETU NA KUHAKIKISHA MIPANGO MAALUMU ILI NCHI YETU IWEPO PIA BAADA YA MIAKA ELFU..
kwa hiyo nahitimiza mtazamo wangu kuwa kabla hatujawanyooshea vidole WACHINA na WAZUNGU tujiangalie sisi binafsi tuna upendo gani kwa nchi yetu na wananchi wetu. Na Tusiogope kuwaambia VIONGOZI wetu kuwa sisi wananchi ndio tunaoweza kuleta maendeleo ya nchi kama TUKIWEZESHWA na TUKAJIWEZESHA na pia tuwaambie usoni bila haya ama kuogopa kuwa UMASIKINI tulionao ni wakujitakia na wao tumewachagua kwa sifa ili watukomboe na sio kutuangamiza. Washughulikie SERA za maendeleo wafukuze wala rushwa na wabadhirifu wa MALI za umma na WASIUZE nchi yetu kwa BEI ya kujinufaisha wao binafsi....
Mdau Mwanafunzi..

No comments: