Monday, 27 June 2011

MTAZAMO WANGU KUHUSU AMANI NA TAHADHARI YA KIFIZIKIA KATIKA NCHI ZA AFRIKA.

Kama mwanafizikia katika masuala ya kiatomiki-asilia (quantum) nimeweza kutambua umuhimu wa amani katika mfumo wa viasili ambapo kuna sheria maalum za kifizikia ambazo hufuatwa. Sheria hizo huhakikisha kuna kuwa na msawazo-suluhishi (homogeneity) kati ya viasili hivyo. Utauliza kweli hayo mkuu? Jibu ni kweli kwasababu japo viasili havipendi kukaa pamoja (fermions) lakini kutokana hali halisi ya mazingira hufikia muafaka wa kuishi pamoja kwa amani hali ambayo hata sisi wanadamu ambao tumetengezwa kwa viasili hivyo tunakuwa katika mazingira ambayo hatuna chaguzi zaidi ya kuishi pamoja kwa amani japo tuna tofauti nyingi.
Kitu kinachotufanya tuishi pamoja ni uvumilivu kati yetu kwa kupuuza tofauti zetu na kuimarisha yale yanayotufanya tuwe kitu kimoja. Katika kuvumiliana ndipo tunapata AMANI lakini UVUMILIVU hutegemea mambo mengi hasa katika jamii yetu ni upatikanaji na ugawanywaji wa mahitaji muhimu ndio hupewa umuhimu mkuu. Kama viumbe wenye fikra tumegawa madaraka kwa kundi la wachache waweze kusimamia mambo hayo na kutuongoza katika kuendeleza hali zetu za maisha.
Uvumilivu ni kama mpira wa manati unapovutika huweza kufanya kazi iliyokusudiwa. Lakini UVUMILIVU unaweza kutafsiriwa kama WOGA katika hali Fulani kwani kama ni foleni basi nyuma ya Uvumilivu ni Woga na mbele yake ni Unyama. Kwa hiyo jamii yeyote lazima itazame kwa uangalifu mipaka ya AMANI inayotokana na uvumilivu. Nchi yetu inasifika kwa kuwa na amani inayotokana na uvumilivu wa hali nyingi hivyo kuifanya nchi yetu iwe ni yenye uvumilivu mkuu kati ya wanajamii na pia kuwa na hatari kuu mara mipaka ya uvumilivu huo ikivukwa.
Nchi yetu ina makabila zaidi ya mia moja na pia kuna wafuasi wa dini mbalimbali pia kuna watu wa rangi mbali mbali na pia upatikanaji wa mahitaji muhimu katika maisha pia yamegawanyika mara nyingi kufuata tofauti tulizonazo. Sitaki kunyoosha kidole kwa kabila, dini ama rangi yeyote lakini ukweli unabaki kuwa tofauti ya walionacho na wasionacho ni kubwa.
Hii inaonekana katika miji yetu mikubwa kuwa kuna tabaka la watu ambalo linaundwa na viongozi waliochaguliwa na wanajamii kuhakikisha kuna masawazo wa upatikanaji wa mahitaji muhimu lakini badala ya kutetea matakwa ya jamii wameelemea kutetea wazi wazi maslahi binafsi. Hali hii ni hatari kwa uwe mvutiko (strain) wa uvumilivu kwa maana ukivuta sana mpira wa manati hukatika na mara nyingi matokeo ni majeraha kwa mvutaji. Hapa nataka kusema kuwa ile simenti inayoshikilia amani inayotokana na uvumilivu inaanza kumemenyuka. Hata katika viasili mvutiko (strain) unapozidi basi hufumka kwa kishindo kikuu ili amani ije ipatikane tena (relaxation to ground state).
Kwa sisi binaadamu ina maana uvumilivu ukipotea jamii itaingia kwenye eneo la unyama ambapo maisha na mali za wanajamii zitapotea kabla ya miaka kupita na kupata suluhu ya kuvumiliana tena. Tumeona hali hii ikitokea kwenye nchi nyingi kama Rwanda na Burundi, Sudani na kwengineko lakini ishara zake zimeanza kujitokeza nchini kwetu, mfano ni mauaji wa watu waliokwenda kuvunja nyumba pale Tegeta, mauaji ya Tarime na kwengineko.
AMANI inayotokana na uvumilivu inatoweka kila siku zinavyopita kiasi sasa naweza kusema sasa tunaingia kwenye amani inayotokana na WOGA. Na cha hatari zaidi WOGA ni hali tete (unstable state) ambayo si vyema kukaa nayo maana WOGA ukitutoka tunarukia kwenye UNYAMA ambao matokeo yake ni mauaji ya halaiki na upotevu wa mali na kurudisha nyuma hatua zote zilizotifikisha tulipo. Tujifunze hali iliyopo LIBYA na kwengineko ambako walikuwa na amani inayotokana na WOGA leo wameushinda WOGA wao na nchi imetumbukia kwenye vita kufuta maendeleo yote waliyopiga.
Sitabiri balaa lakini kwa mwenye akili ya kusoma nyakati atatambua kuwa tunaelekea huko kwenye balaa hali tunajua taathira yake. Leo hii vyama vya siasa vimekusanya ushawishi mkubwa kwa wananchi ambao hali zao ni duni badala ya kuweka maslahi ya wananchi mbele wameweka maslahi yao binafsi mbele zaidi kiasi maisha ya mwananchi wa wakaida yamekuwa magumu mara nyingi zaidi ya miaka iliyopita. Uchaguzi unaokuja 2015 utakuwa ni mtihani mkuu wa AMANI tuliyonayo.
Leo hii Wazazi wanashindwa kulea watoto wao hivyo watoto omba omba wanazidi kuongezeka. Wazazi wanashindwa kusomesha watoto. Vitendo vya kihalifu vinazidi kuongezeka na hivi ndivyo vitakavyoondoa WOGA na kututumbukiza katika janga. Zamani wananchi hawakujua nini kinachoendelea lakini dunia ya leo yenye mitandao na njia nyingi za mawasiliani zimefumbuwa macho na masikio ya wengi na hivyo ni jukumu la viongozi wetu kujua kuwa matokeo huwa ni vitendo vilivyofanywa kabla (CAUSALITY).. ili tupate matokeo mema tubadilishe vitendo vyetu vya sasa na kutimiza majukumu yetu kwa faida ya TAIFA letu na Wananchi wetu. Hoja zenye kutetea wananchi zinaposhindwa bungeni kwa utashi wa siasa ujue ndio chachu ya kutokomeza WOGA uliopo na kulikurubisha taifa katika uvunjifu wa AMANI.
Ndimi Mdau Mwanafunzi

No comments: