Sunday, 3 July 2011

TUNAJENGA NYUMBA YA MAENDELEO ISIYO NA MSINGI

Nyumba imara huanza kwenye mipango (plan) maalum inayozingatia vipengele muhimu vitakavyotumiwa ili nyumba itakayojengwa ihimili purukushani za maisha ya kila siku ya mtumiaji wa jengo hilo. Na nyumba imara huanzwa kwa kujenga msingi ulio imara uliothibitika kuweza kubeba uzito wa kuta na paa la nyumba na vitu vitakavyokuwemo na watumiaji wa nyumba hiyo. Nyumba ninayozungumzia hapa ni mfumo mzima wa maisha ya mtanzania na mazingira yake. Wote tunajua kuwa ili tuweze kupata maendeleo ya kweli lazima tuweke msingi imara wa maendeleo hayo.

Maendeleo yako mengi tunaweza kuyapima kwa kutumia kigezo cha muda kama kuna tofauti kati ya muda uliopita na wasasa basi kuna maendeleo. Maendeleo yanaweza kuwa chanya ama hasi. Kama tofauti iliyopo ni bora kuliko tulipoanzia basi tuna maendeleo chanya na kama hali ya sasa ni mbaya zaidi ya iliyopita basi tuna maendeleo hasi ama tunapiga hatua za kurudi nyuma badala ya kwenda mbele.
Tanzania tunahitaji maendeleo katika Nyanja nyingi tofauti kuanzia nyumbani mpaka makazini. Ni lazima tuamshe fikra zetu kuelewa tulipo na wapi tungependa tuwepo. Naamini wote tunapenda kuishi maisha bora kama tunayoona kwenye TV zinazoonyesha vipindi vya nchi za n’gambo japo mimi nisingependa tuishi kama kopi ya maisha ya TV hizo kwasababu tuna mengi ambayo ni vyema kujivunia na utamaduni ni moja ya mambo muhimu kuyashikilia na kuyaendeleza kwa mtazamo wetu wenyewe badala ya kushurutishwa mabadiliko na wageni. Lakini wengi wetu hatuna muda hata wa dakika moja kufikiri kwanini tupo katika hali hii na tufanye nini kuibadilisha. Wengi wetu huamini maisha bora huja kwa ngekewa ama njia za mkato ambazo wengi wenu mnazijua.

Wengi wetu tumegubikwa na giza la UBINAFSI linalotufanya tusiweze kuona jukumu la mchango wetu na wenzetu katika kubadilisha jamii inayotuzunguka Giza la UBINAFSI huanzia nyumbani na kuhamia makazini na serikalini na kutanda nchi nzima. Ubinafsi unatufanya tusiweze kutoa nafasi kwa yeyote mwengine zaidi yetu.

Nikirudi kwenye misingi bora ya nyumba ya maendeleo lazima kwanza niweke wazi kuwa mipango (Planning) na vitendo(action) ndio chanzo cha mafanikio. Wengi wetu tna mipango mingi na serikali yetu ina mipango mingi lakini vitendo ni tatizo kubwa. Wengi wetu hupanga lakini mara nyingi hupangua na kuamua kutotekeleza mipango yetu. Na serikali yetu imepanga mambo mengi lakini utekelezaji wa mipango hiyo hakuna. Mipango imebaki kwenye makabati ya kuhifadhia nyaraka ikioga vumbi. Na hata hiyo ambayo inayotekelezwa basi utekelezaji wake ni asilimia chache inayoshabihiana na mipango ya awali.
Kwa hiyo tumekosa watendaji na pia tumekosa wahakikishaji wa vitendo hivyo. Tunasheria nyingi lakini ubabe ndio unaotawala maamuzi yetu. Na hii inaonekana zaidi katika serikali kufanya uwekezaji toka nje ndio sera namba moja. Tunatumia mali nyingi kuliko faida itakayopatikana kuwavutia watu wa nje waje kuwekeza kwenye nchi yetu wakati kama ni uchimbaji wa madini hata hayo makampuni makubwa yalianza kwa kuchimba kwa kutumia sururu na matoroli na wakajiendeleza kielimu na kimsingi mpaka wakaweza kununua mashine za kuchimbia na magari ya kusomba mawe. Sasa kwanini na sie tusianze huko kwa kuendeleza kampuni za ndani ya nchi ambazo tuna uhakika wa kuunda ajira ya ndani na pia kujenga teknolojia ya ndani ambayo itahakikisha kuwa ajira inakuwa na utaalamu unazidi na pia pato linabaki ndani ya nchi na hayo ndio maendeleo ya kweli. Kwa nini tunapenda kuwa na ustawi wa tawi kutoa maua bila ya shina na mizizi.

Na msisitizo ni kwamba si ukweli kuwa hakuna watekelezaji ila hawapewi nafasi na kizingiti kikubwa ni ubinafsi uliopo. Hatupeani nafasi ya kujikuza na hatuna upendo wa kweli chuki na ubinafsi ndivyo vinavyotawala nafsi zetu, tunapenda kuona wenzetu wakiwa na tabu hatupendi kuona jirani ana hali nzuri zaidi yetu tunapenda sie tuwe juu zaidi. Na kama watu wana sifa za ubinafsi na chuki hata serikali inakuwa na sifa hizo kwasababu serikali ni mkusanyiko wa watu. Kwa hiyo chuki na ubinafsi zinatawala katika maamuzi muhimu ya taifa. Mfano ni hivi karibuni ambapo viongozi wetu wanasema hadharani kama pesa iliyoamuliwa kurejeshwa kwa wananchi wa Tanzania haitapelekwa serikalini basi watazuia hao watakaopewa pesa kunufaisha wananchi..kauli hii inaonyesha chuki na ubinafsi uliopo. Badala ya kuwa hii ni ushindi kwa jamii (WIN WIN situation) imekuwa bora tukose sote.

Na sasa viongozi wanataka kuruhusu kampuni za kigeni kuchimba madini ya Uranium katika mbuga ya Selous, kampuni zitakazochimba zinategemea kupata dola milioni 200 kwa mwaka na kuigawia serikali dola milioni tano ambapo ni sawa na asilimia mbili na nusu ya mapato. Je asilimia mbili na nusu inatosha kudhibiti uharibifu wa mazingira utakao tokana na uchimbaji wa madini haya ya hatari. ni Kweli tunataka kuendeleza uchumi lakini tunapapatikia vijichenji wakati noti tunawaachia wageni wakizipeleka kwao huku tukibaki na mashimo na madhara kwa mazingira na kwa watu na wanyama wanaozunguka machimbo.

Tunapenda njia za mkato bila kazi ngumu tunataka mambo ambayo yameshatengenezwa (ready made) wakati tunajua kuwa nchi zilizoendelea hazikuendelea kwa njia ya mkato kwa nini sisi tuweke njia ya mkato mbele. Njia ya mkato ndio inayofanya majumba yakaporomoka na hivyo hivyo uchumi wa nchi kudorora na kudumaa na kuwaacha wananchi wakiwa katika hali mbaya.

Inaonekana kama kwamba viongozi wako katika haraka ya kumaliza malighafi tulizonazo kama vile hawatarajii nchi hii kuwepo baada ya miaka mingi inayokuja. Ni kama hawajaelewa kuwa malighafi ndio itakayofanya nchi kuwa na nafasi katika mataifa siku zijazo. Ni kama mfanyabiashara mwenye kuuza mali zake kwa bei ya chee haraka apate kuhama. Nchi yenye kuelewa misingi ya maendeleo kwa mfano Marekani ni nchi yenye mafuta mengi kuliko zote duniani lakini wao ndio wanunuzi wakuu wa mafuta kutoka nchi nje. Inaonyesha jinsi walivyo na mipango ya nchi yao kujikimu kimahitaji miaka mingi inayokuja.

Msingi bora wa maendeleo ni kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika kila hatua ya kujenga nchi na kuleta mabadiliko ambayo yanatokana na mikono yao wenyewe. Na nyumba isiyo na msingi si imara na hatimaye huporomoka.

No comments: