Thursday 6 September 2007

Ningelikuwa Mwalimu MKUU wa Shule...

Ningehakikisha kwanza majengo ya shule ni ya kuvutia ya na Milango na Madirisha, kuta zimepigwa rangi na pia madawati ya kutosha kwa kila darasa. Pia darasa lisizidi wanafunzi Arobaini na tano. ningehakikisha kuna Maktaba ya Vitabu na Vitabu vya kutosha kwa ajili ya wanafunzi na walimu. Kuna Viwanja vya michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu(football), Kikapu kwa waume na wanawake(basketball and netball), pia na riadha. hakikisha walimu wako na elimu inayokwenda na muda kwa kuhamasisha upitiaji wa majarida ya kisasa yahusuyo elimu ya nadharia na pia vitendo. ningehakikisha kuna Maabara na pia karakana kwa ajili ya mafunzo ya vitendo yakiwemo ya ujenzi, seremala, uchongaji, kilimo, ufugaji, ufundi wa magari, vitu vya elektroniki na aina zote za ufundi ambazo hawa wanafunzi wakimaliza shule wawe na uwezo halisi wa kujitegemea. ningehakikisha walimu wanalipwa mishahara yao kwa wakati muafaka, pia wanapongezwa kwa juhudi binafsi wanazojitolea. ningeweka mkazo maalum katika kuhakikisha jamii inayozunguka shule hiyo inafaidika na pia shule inafaidika kutokana mahusiano mazuri kati ya shule na jamii husika. ningehakikisha wanafunzi wanawekewa mazingira ya kuipenda shule na kusaidia wanafunzi wasio na uwezo kupata elimu sawa bila ubaguzi wa aina yeyote ile. ningehakikisha kuna heshima na maadili bora ya kazi kwa wote wanafunzi na walimu pia. ningehakikisha kuna safari za kimafunzo kama kutembelea mbuga za wanyama ili kujifunza mahusiano ya binadamu na wanyama mwitu pia uhifadhi wa mazingira, kutembelea viwanda kujifunza jinsi bidhaa zinavyozalishwa na pia mashine zinavyofanya kazi. kuweka mashindano ya ubunifu wa vifaa na vitendea kazi, uboreshaji huduma na mambo mengi ili kuibua mawazo mapya kusaidia jamii kujikwamua toka kwenye matatizo yanayoikabili.

No comments: