Tuesday, 17 May 2011

Usafiri wa Mbagala Kilakshari

Nimeona niitafsiri hii maana kila nikiisoma nacheka mbavu sina:
Utakuwa mshamba kama hujawahi kupanda daladala aina ya DCM toka kigamboni kwenda Mbagala rangi tatu! Kweli we utakuwa unatoka dunia nyengine kabisaaa!! Hujafika BONGO kwa nini usikatae na kuniona mie muongo ili ukapande daladala toka Feri kwenda Mbagala au Feri Mwenge au Kariakoo kuelekea Bunju. Basi siku moja nikaamua kwenda kutembea Mbagala kupitia feri kuzurura si unajua Utalii sio mpaka uende Manyara, Selous ama Serengeti.. Tripu nzima ni Buku mbili na pesa ya juisi na mihogo ya kuchoma.

Basi nikapanda daladala DCM limechoka na limejaa ile mbaya huku moshi umezingira basi zima. siku hesabu lakini tulikuwa kama watu 80 kwenye basi la abiria 40. Hapa ndio BONGO, wasafiri wengine wanapanda kupitia madirishani wengine mlangoni basi ili mradi usivae shati jeupe utafika unakokwenda likiwa jeusi kwa magirisi na shombo za samaki. lakini hii si ajabu kwa wakazi wa Mbagala washazoea.. Wengine wanakula vipande vya miwa, kuna wakinamama na mabeseni yao ya samaki, wengi wao ni samaki aina ya chuchunge, Msimu wa chuchunge babu...wengine wanakula machungwa na wapitisha pweza madirishani wanauza juu kwa juu.
"Lete Pwezaa bwana dawa ya chakula cha usiku hao"...
Kuna jamaa wanavuta sigara na hakuna anayethubutu kusema Neno..Sema kitu uishie kulazwa muhimbili na majeraha ya kichwa na pengine upate tetnus ukipona we unabahati.
Basi lilijaa lakini Konda kakazana kusukuma watu wajae zaidi huku akitangaza

"KUNA NAFASI ZA KULALA !!! SITI KIBAAAAAOOO, GARI HAIJAI INAJAA NDOO YA MAJI!!!"

Kuna jamaa wako juu ya gari washalipa nauli kabla ya kuruhusiwa kupanda ngazi kuelekea mbinguni..Baada ya dreva kuridhika kwamba mlango haufungiki kwa watu kujaa tukaanza safari ndani la gari la maraha kuelekea MBAGALAAAAAA!!!.
Basi linanuka moshi wa sigara, Pombe, samaki na moshi mchafu wa gari..watu wakaanza maneno kama ndege kwenye tawi la muwembe.

"We dada uwe unanyoa j amani !!! Mrembo mzuri lakini kikwapa kinanuka!!!" "Mpashe huyooo...kasuka nywele utazania kalambwa na ng'ombe!!! Eti ndio katoa shilingi alfu saluni! mie kama ni mke wangu namnyoa usiku...zooote akiamka kama kibwengo!!"

"Mrembo gani huyu hebu mwone midomo kama subiani...hivi anajiona kapendeza sanaaaa!!! Eti wanaiga wazungu lipustiki!!!" " Kama ni mke wangu wallah nakuapia talaka saba!!! Ati anajifanya misstanzania ...kumbe kalalia mlo wa mhogo na mchicha!!!"

Nikajua hapa kitanuka sasa hivi kuna chungu kinapikwa. Kuna mzee wa makamo kwenye siti ya nyuma akaanza kutapika, harufu balaaa..

"Eheee!!! gongo la kigamboni hilo !!!." Kwani Kigamboni kuna gongo la bure??? Pesa yangu nakula...nitakutoa nishai... Wee kama huna hela shauri lako macho kama kenge kasoro mkia etcetc.

sie wengine tukanyamaza kimya kama hatujasikia kitu tusije tukajeruhiwa kwa kosa la mropokaji.
mara kidogo:

We mama mbona unanikalia? na minguo yako imelowa misamaki???unajua bei ya hii suruali yangu?? Umewahi kukaliwa weee,koma kabisa!!! kama una ubavu si ushuke ukapande taxi??? Wee mama si ungepanda ungo,mwanga mkubwa wee!!!

matusi yakazidi kuporomoshwa tukajikuta kituo cha polisi cha Kilwa Road Sio kwa ajili ya matusi bali Konda ambae anaonekana kakimbia umande zamani kuna jamaa anajidai kalala hataki kulipa nauli. konda kumuamsha alipe nauli ikawa kosa. Mwanaharamu jicho jekundu kwa Bangi na harufu nzito ya Gongo la kigamboni kaja juu.

"SILIPI NAULI sina SHILINGI NA UNAWEZA KWENDA POPOTE"

..KONDA akamuacha akakusanya nauli kwa waliotaka kulipa halafu akamrejea jamaa wenye jicho kama shetani. Konda miraba minne akamkunja jamaa huku akidai nauli...Ohhooo Jamaa kachomoa kisu na Konda katoa BISIBISI, wengine tunaangukiana tukijiepusha tusijechomwa na bisibisi ama kisu..
DEREVA peleka gari polisi kuna chizi hataki kulipa nauli halafu ana kisu lazima aende selo huyu..
Bahati tulikuwa karibu na kituo cha polisi Kilwa Road. Ikabidi dereva apeleke daladala lilijaa kupita kiasi kituoni.. Kuna jamaa akasema
"hivi kweli abiria tunapelekwa polisi kwa ajili ya shilingi mia mbili tu?? Mimi nitamlipia!"
lakini basi lilishaingia kituoni. Kuna afande akaja kuuliza kulikoni.. "Afande kulikuwa na Chizi hataki kulipa lakini mimi nitamlipia!
"HEE MMEKUJA KWENYE MAONYESHO YA FASHION HAPA KITUONI..SHUKENI MMOJA MMOJA TOKENI HARAKA.. WE DREVA NENDA KAANDIKE RIPOTI KULE NDANI"
Yule afande akakaripia..
"Mmekuja kuuza sura hapa? gari imejaa kama ile ya Mererani, nanyi abiria mnakubali kupangwa kama sangara!!!Halafu unadhani utaondoka hivi hivi tu hapa? Gari yako kwanza ni mbovu na hii ni wiki ya usalama haijakaguliwa hii!!!"
Yule jamaa aliyetapika hakushuka akaachwa anakoroma ndani ya daladala.. Baada ya saa nzima na bonge la tabasamu la wale afande tukaruhusiwa sikujua nini kilichowafurahisha kiasi cha kutuaga "MWENDE SALAMA"..HIVI yale mabasi ya KASI yakowapi ama nilikuwa ndotoni tu???

No comments: